Shirika lakusanya saini kupiga marufuku Kilimo cha Kiwandani

Shirika lakusanya saini kupiga marufuku Kilimo cha Kiwandani

NA SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Kuangazia na Kutetea Haki na Maslahi ya Mifugo na Wanyapori Duniani (WAP) linakusanya saini kushinikiza serikali za mataifa ulimwenguni kupiga marufuku mfumo wa Kilimo cha Kiwandani.

Maarufu kama Factory Farming kwa Kiingereza, ni mfumo wa kufuga idadi kubwa ya wanyama wa nyumbani ili kuafikia mahitaji ya nyama sokoni.

Kupitia kanuni zilizowekwa, walioukumbatia wanapunguza gharama kwa minajili ya kuwahi faida nono.

Ikitahadharisha kuhusu mfumo huo, WAP imesema ni mojawapo ya viini vya uchafuzi na uharibifu wa mazingira, na zaidi ya yote kuchangia tabianchi.

Kulingana na shirika hilo, unachangia utoaji wa gesi hatari ya Kaboni.

Ni kutokana na athari hizo, WAP inaendeleza kampeni dhidi ya mfumo huo hatari.

Kampeni zinazokusanywa na shirika kwa ushirikiano na wadauhusika, zitakabidhiwa viongozi wakati wa Kongamano la Umoja wa Mataifa Kuhusu Tabianchi Mwaka huu, COP27.

Hafla hiyo inayolenga kujadili mikakati kukabiliana na tabianchi, itafanyika nchini Misri mwezi Novemba.

“Hatuna budi ila kukomesha Kilimo cha Kiwandani,” akasema Bw Tennyson Williams, Mkurugenzi Mkuu WAP Afrika akizungumza jijini Nairobi.

Tayari, baadhi ya wadauhusika kutoka sekta ya kibinafsi na umma wametangaza kuunga mkono mswada huo ili kuokoa mazingira.

“Tunaunga mkono hamasisho kutunza mifugo, hususan kuku kwa njia ifaayo,” akasema Bw Jim Tozer, Mkurugenzi Mkuu Kenchic Ltd.

Kenchic ni kampuni tajika katika uzalishaji wa kuku.

Kulingana na WAP, kwa nia ya kupata mafasi zaidi kuendeleza ufugaji miti na misitu inaharabiriwa, dawa zenye kemikali zinatumika suala ambalo linahatarisha mazingira.

Isitoshe, kufuatia msongamano wa mifugo kinyesi kinakuwa balaa kudhibiti.

Linataja hatua hiyo kama uharibifu wa mazingira.

“Lazima tukomeshe ukatili kwa mifugo na wanyamapori,” Bw Williams akasisitiza.

Afisa huyo alisema uharibifu wa misitu unachochea upungufu wa wanyamapori, makazi yao yakivamiwa.

  • Tags

You can share this post!

Wenye vipande vya ardhi Diani waonywa kupoteza endapo...

Yaya asukumwa jela miaka 5 kwa kumlisha mtoto kamasi

T L