Habari

Shirika lasaka wanaume 100 kushiriki mpango wa kupanga uzazi

April 19th, 2018 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WANAUME wanaotaka kupanga uzazi wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kukatwa mishipa ya kusafirisha mbegu za kiume kwa lengo la kuwakinga dhidi ya kupata watoto zaidi.

Kampeni hiyo ya kuwakata wanaume mishipa ya kusafirisha mbegu za kiume, maarufu vasectomy, inatarajiwa kuzinduliwa Ijumaa jijini Nairobi lakini shughuli ya kuwasaidia wanaume kupanga uzazi itang’oa nanga Jumatatu, Aprili 23 had Aprili 26, mwaka huu.

Kampeni hiyo inaendeshwa na shirika lisilo la serikali Family Health Options Kenya (FHOK) ambalo limetangaza kuwa linalenga kufanyia upasuaji wa mishipa ya kiume wanaume wasiopungua 100.

Kampeni hiyo ya siku nne itaambatana na maadhimisho ya Siku ya Vasectomy Ulimwenguni (WVD).

Jijini Nairobi, upasuaji huo utafanyika katika kliniki ya FHOK iliyoko Jumba la Phoenix, Barabara ya Kenyatta.

Kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, kampeni hiyo itaendeshwa na madaktari wawili kutoka Amerika, Dkt Doug Stein na Dkt John Curington wanaofanya kazi na shirika la No Scalpel Vasectomy International (NSVI).

Madaktari hao wataongozwa na mtaalamu wa kupanga uzazi kupitia ukataji wa mishipa ya kusafirisha mbegu za kiume nchini Kenya Dkt Charles Ochieng.

Kulingana na mwandalizi wa kampeni hiyo Mark Sennah Akoi, huduma za vasectomy zitatolewa bila malipo na wahusika pia watasafirishwa bure.

“Tuna matumaini kuwa tutapata angalau wanaume 100 jasiri watakaojitokeza kukatwa mishipa ya kusafirisha mbegu za kiume,” akasema Bw Akoi.

“Wanawake wana zaidi njia 10 za kupanga uzazi lakini waume wana mbinu mbili pekee ambazo ni utumiaji wa mipira ya kondomu au ukataji wa mishipa ya kusafirisha shahawa (sperms) yaani vasectomy,” anasema Dkt Ochieng’ anayefanya kazi na Winam Safe Parenthood Initiative (Wispivas).

 

Fomu ya kukubali

“Kabla ya kufanyiwa upasuaji huo mhusika anapimwa afya yake na kupewa maelezo kuhusiana na huduma hiyo na kisha anatia saini fomu ya kukubali kwa hiari kukatwa mishipa ili kupanga uzazi,” anaongezea.

Vasectomy inazuia mbegu za kiume kumfikia mwanamke wakati wa kufanya mapenzi lakini haizuii mwanaume kufanya kitendo cha ngono, kulingana na Dkt Ochieng’.  Vasectomy imethibitishwa kuzuia mimba kwa asilimia 99.

Wakati wa kampeni iliyoendeshwa mnamo 2016, zaidi ya wanaume 74 walijitokeza kufanyiwa vasectomy.

Kampeni hiyo, hata hivyo, imekumbani na pingamizi kali katika mitandao ya kijamii huku wengi wa wanaume wakisema kuwa hawako tayari kufanyiwa vasectomy.

?”Mke akitaka kukuacha anakushauri kwenda vasectomy na baada ya miaka miwili anakwamba anataka mtoto, kwa sababu huwezi anaondoka na kukuacha,”  akasema Morrison Mutinda katika mtandao wa Twitter.

Naye, Anthony Mwangi alisema: “Itakuwaje, mama watoto akitoroka na watoto wote ilhali nimefanya vasectomy? Wanaharakati waachane nasi.”