Shirika latilia shaka maandalizi ya IEBC

Shirika latilia shaka maandalizi ya IEBC

WACHIRA MWANGI na FARHIYA HUSSEIN

SHIRIKA moja la wanaharakati nchini limeelezea wasiwasi wake kuhusu maandalizi duni miongoni mwa taasisi muhimu zilizotwikwa jukumu la kusimamia chaguzi.

Kundi hilo lionalojumuisha wananchi na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kwa jina Angaza Movement limelalamika kuwa taasisi hizo zimetekwa na maslahi mbalimbali yanayoegemea serikali na makundi mengineyo hivyo kuendeleza utamaduni wa ufisadi. Akihutubia vyombo vya habari katika Kaunti ya Mombasa, Mkurugenzi wa Tume ya Kimataifa kuhusu Majaji (ICJ Bi Elsy Sainna alisema kuwa wanatilia shaka kuwepo kwa uhuru na haki katika chaguzi zijazo mnamo Agosti.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitangaza rasmi Jumanne, Agosti 9, 2022, kama tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa tatu chini ya Katiba Mpya ya Kenya, 2010.

Alisema kuwa kwa kutoa kalenda ya uchaguzi, IEBC ilinuia kuwahakikishia Wakenya kuwa Uchaguzi Mkuu ujao utakuwa huru, wa haki na kweli jinsi inavyohitajika kikatiba.

“Kila uchaguzi Kenya umekuwa ukivurugwa tangu 2007. Kenya bado imebebeshwa mzigo wa chaguzi tata ambazo hazijasuluhishwa jambo ambalo limeathiri pakubwa imani ya umma kuhusiana na uadilifu wa mchakato wa uchaguzi,”

“Utendakazi wa IEBC katika usajili unaoendelea wa kusajili wapiga kura unaoambatana na sajili za wapiga kura zinazokumbwa na hitilafu kila mara hauvutii imani kwamba uchaguzi utakuwa huru, wa haki na wenye uadilifu,” alisema Bi Sainna.

Walisema kuwa taasisi za IEBC, vyama vya kisiasa, bunge na serikali zinaendelea kukiuka Katiba na korti kuhusu ujumuishaji wa wanawake vijana na walemavu.

“Uchaguzi unaofanyika katika hali hiyo huwezi kutajwa kama ulio huru, wa haki na wenye uadilifu. IEBC na mashirika mengine ya kitaifa yamekataa kimaksudi kuzingatia na kutekeleza masharti yanayohitajika kuhusu uadilifu. Imefeli au imekataa kusisitiza demokrasia katika vyama vya kisiasa vinavyofadhiliwa na umma kwa kuvitaka kutimiza masharti ya kikatiba kuhusu uwazi na uwajibikaji kwenye michakato yao ya kisiasa,” alifafanua.

Kundi hilo linaamini kuwa IEBC na taasisi nyinginezo zimetekwa na maslahi ya kisiasa yanayodumaza maslahi, usalama, ulinzi na demokrasia ya wananchi.

 

You can share this post!

Sapit: Msiwachague wasiotekeleza ahadi

TUSIJE TUKASAHAU: Badi asije akasahau kuwa karibu hospitali...

T L