Makala

Shirika lawashawishi wanawake kujiepusha na biashara ya 'nipe ngono nikupe samaki'

February 7th, 2020 3 min read

Na GAITANO PESSA

IDADI kubwa ya wanawake wanaoishi karibu na fuo za Ziwa Victoria, Magharibi mwa nchi wanajihusisha na biashara ya samaki ambayo ni njia mojawapo ya kujipatia kipato ili kukidhi mahitaji ya kila siku.

Katika Kaunti ya Busia, zaidi ya wanawake 1,000 wanahusika moja kwa moja na biashara hii iliyonoga katika fuo 20 zinazopakana na ziwa hilo.

Hata hivyo, katika uuzaji huu wa samaki, baadhi wamejipata wakitumia njia za mkato kupata samaki kutoka kwa wavuvi; hasa “nipe ngono nikupe samaki”.

Idadi ya samaki imekuwa ikididimia kutokana na uvuvi mbaya na vilevile mabadiliko ya tabianchi.

Hii ndiyo sababu shirika lisilo la serikali la Anglican Development Service (ADS) limekuwa mstari wa mbele kuwapa uhamasisho dhidi ya mienendo ya aina hiyo ambayo ni hatari.

Mshirikishi wa ADS katika eneo hilo Chrispinus Mang’eni, anasema wamefaulu kuwahamasisha zaidi ya wanawake 8,000 dhidi ya biashara hiyo hatari katika fuo tano za Samia.

“Tuna zaidi ya maafisa 60 wanaofanya uhamasisho katika fuo hizi kuhakikisha tunawashawishi wanawake hawa kuepukana na biashara hiyo ama watumie kinga iwapo wana wapenzi zaidi ya mmoja ili kuepuka maambukizi,” akasema Bw Mang’eni.

Mradi huo wa ADS pia unahusisha kuchunguzwa kwa wanawake dhidi ya saratani ya kizazi – cervical cancer – ambayo imekithiri sana katika eneo hilo.

Mshirikishi wa ADS eneo la Busia Chrispinus Mang’eni. Picha/ Gaitano Pessa

Usemi wa Mang’eni uliungwa mkono na afisa wa afya ya nyanjani wa ADS Bw David Olali aliyefichua kuwa tangu kuanzishwa kwa mradi huo wengi katika Jamii wamejitokeza kufahamu hali yao ya HIV.

“Ubadilishanaji wa ngono kwa samaki ni biashara hatari kwa sababu Ukimwi husababisha vifo, lakini pia unyanyapaa na baadhi ya waathirika kuishi katika hali ya kutojikubali inayowanyima fursa ya kutafuta matibabu,” akaonya Bw Olali.

Akaongeza: “Tunataka wanawake wainuke kwa faida ya Jamii na familia zao. Nina furaha kuwa mradi huu polepole unaafikia malengo yake.”

Bi *Jane ambaye jina lake tumelibana, amefanya biashara hii kwa zaidi ya miaka 10; muda huo wote akishiriki ngono na zaidi ya wavuvi watano kupata samaki.

Ni siri ambayo mumewe hakutambua na baadaye akaishia kuambukizwa virusi vya HIV vinavyosababisha Ukimwi.

Matukio haya anasema yalibadilisha maisha yake milele.

Upepo mtulivu wa ziwa unatukaribisha katika ufuo wa Bumbe katika eneobunge la Funyula, kaunti ya Busia.

Bado ni saa mbili asubuhi lakini tayari biashara imenoga kwelikweli wengi wa wafanyabiashara hapa wakiwa wanawake.

Madau yaliyotengenezwa kwa mbao yametoka visiwa vya Sigulu, Hama, Wayasi, Lolwe na Sumba maarufu miongoni mwa wavuvi kutokana na idadi kubwa ya samaki aina ya ngege na mbuta wanaopatikana katika maeneo haya.

Kila mara dau linapowasili wanawake kadha wanalizingira na kung’ang’ania samaki wanaoutupwa kwa mitungi ya plastiki yenye maji.

Hata hivyo *Jane, 48, anaonekana kuibuka na samaki wengi kila mara anapotoka katika dau.

Uhusiano wake na wavuvi unaonekana mzuri sana kutokana na tabasamu na vicheko vinavyopasua angalau akiwa nao.

Kutoka na uhaba wa samaki, *Jane anasema alilazimika kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na wavuvi kuimarisha biashara yake. Ni mama ya watoto watano.

Japo alibadili mienendo baadaye, anasema biashara hii ingalipo kwa wingi.

“Unapojiingiza katika biashara hii ya kuuza samaki unafaa kuweka kando maadili na kuwa tayari kuuza mwili wako kingono ili kupata samaki la sivyo utaambulia patupu,” asimulia *Jane.

Anasema alishiriki ngono na mara nyingi bila kinga.

“Yote haya yalifanyika kisiri mgongoni mwa mume wangu kwa sababu wapenzi wangu wengi tulikutana katika madanguro mchana mbali na nyumbani,” anahadithia.

Hata hivyo maisha yake yalichukua mkondo mpya mwaka wa 2012 alipotembelea hospitali ya misheni ya Nangina baada ya kujihisi mnyonge.

Alipofanyiwa vipimo alipatikana na virusi vya HIV. Anasema moyo ulimgonga asijue la kufanya ila kutoka kituoni kwa haraka bila kusubiri uhamasisho ilivyo desturi.

Lakini baada ya siku chache alirejea katika mahusiano yake ya kawaida kwa kichochezi kuwa mahitaji ya familia yalizidi virusi vya HIV na hivyo hakuona haja ya kujilinda.

“Kweli nilifahamu fika nilikuwa na virusi na nilihitaji kubadilisha tabia yangu lakini mahitaji ya familia yalinichochea sana nikazidi kushiriki ngono na wavuvi,” akasema.

Matukio haya vilevile yalimtupa katika mizani ya kutojikubali na akasusia kabisa kuorodheshwa miongoni mwa wale wanaomeza tembe za kupunguza makali; ARVs.

Wakati akizidi kucheza, shirikika hili la ADS lilifika katika eneo hilo kwa minajili ya kuwahamasisha wanawake kuhusu athari za biashara hiyo kubadilishana ngono na samaki kando na umuhimu wa kujua hali yao ya HIV.

Ni hapo ndipo mwanamke huyu aliamua kushiriki baadhi ya vikao ya ADS baada ya kushawishiwa na rafiki yake.

“Mradi huu ulinipata nikifanya maovu, lakini baada ya vikao kadhaa nikaamua kufika zahanatini mwaka 2013 kuthibitisha hali yangu na nikapewa mawaidha ya kuishi maisha bora na kumeza tembe za ARV,” akasema.

Mwanzoni hakumfahamisha mumewe lakini baadaye akafanya hivyo. Mume alipatikana yuko sawa kiafya.

Anasema mumewe alimsamehe kwa tabia yake ya awali.

Anawataka wanawake kujiepusha na tabia hii, lakini pia akiwashauri wavuvi wanaume wawe wakifanya biashara halali kwa kuzingatia maadili.

Wizara ya Uvuvi inakadiria zaidi ya wanawake 20,000 wanajihusisha na biashara ya samaki katika kaunti zinazopakana na Ziwa Victoria huku biashara hii ya ngono kwa samaki ikihusishwa na ongezeko la maambukizi ya HIV.