Habari Mseto

Shirika linalodaiwa kulaghai raia lajitetea

August 20th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

SHIRIKA lisilo la serikali ambalo limelaumiwa likidaiwa kuwalaghai wananchi sasa limejitokeza kusema kuwa shughuli zao ni halali.

Shirika hilo kwa jina East Africa Sub-Sahara Safe Promotions Foundation-International (SSASPF) limedaiwa kuwalaghai wananchi katika sehemu mbalimbali kupitia watu wenye mapato madogo kama vile vikundi vya akina mama.

Akiwahutubia wanahabari siku ya Jumanne, mkurugenzi mkuu Julius Kithome amesema kuwa shirika hilo ni halali na kuwa limesajiliwa chini ya sheria za ‘Societies Act’.

Kulingana na Bw Kithome, shirika hilo ni la kidini na lilianzishwa mnamo mwaka 2013 kwa madhumuni ya kuwaunganisha wakenya na kuhubiri.

“Tuligundua kwamba hatuwezi kuhubiri na kuwapa Wakenya chakula cha kiroho ilhali hawajatosheka na chakula cha mwili,” akasema Bw Kithome.

Mkurugenzi mkuu wa SSASPF Bw Julius Kithome (kati) akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi. Picha/ Magdalene Wanja

Mnamo mwaka 2015, shirika hilo liliwashangaza wengi lilipojitokeza na kudai kwamba lingewapa nafasi za kazi zaidi ya Wakenya 20,000.

Jibu hili lilitokana na madai kwamba shirika hilo limerejea tena kwa kuwapa mikopo watu bila riba na ambayo ni ya kati ya Sh100,000 na Sh 1 milioni.

Bw Kithome amefafanua kwa kusema madai hayo ni ya uongo na yanatokana na watu ambao “wanaonea wivu shirika.”

Bw Kithome pia ameonyesha stakabadhi za usajili huku akidai kuwa serikali iliwafanyia uchunguzi wa kina kabla ya kuwapa cheti cha usajili.

“Kufikia sasa tunafanya kazi katika kaunti zote 47 na tuliwaandikia makamishna wa kaunti zote kabla ya kuanza kazi na tukapewa idhini,” ameongeza Bw Kithome.

Bw Kithome pia ameweka wazi kwamba ofisi zao ziko katika mtaa wa Garden Estate ambapo ndipo makao makuu.