Shirika linavyohangaishwa na wanyakuzi wa ardhi

Shirika linavyohangaishwa na wanyakuzi wa ardhi

Na SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Mifugo Nchini (DVS) lilizinduliwa mwaka wa 1895 na serikali ya mkoloni. Uzinduzi wa taasisi hii ya kiserikali ulilenga kuangazia usalama wa mifugo na binadamu katika mazingira.

Likiwa na zaidi ya miaka 120, DVS na ambayo iko chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Wanyama wa Majini, ina jukumu kuhakikisha wanyama wa nyumbani wanalindwa.

Shirika hilo lina matawi kadha sehemu mbalimbali nchini, na hutoa huduma kwa mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda, ngamia, kuku na nyuni, wanyama wa majini na wanaofugwa nyumbani, kati ya wengineo wengi.

DVS pia hutoa huduma kwa wafugaji wa nyuki nchini.

Licha ya utendakazi wake na ambao unalenga kuhakikisha mifugo na binadamu ni salama, shirika hilo liko katika hatari.

Huku Rais Uhuru Kenyatta akiapa kuangamiza ufisadi nchini na kuchukulia hatua kali mafisadi, kufuatia sakata za ubadhirifu wa mali ya umma ambazo zimesheheni katika sekta mbalimbali za serikali, ardhi ya DVS imekodolewa macho na hatari ya wanyakuzi.

Mbali na kunyakuliwa, ncha zake zimeingiliwa na wahuni, wakitafuta mianya ya kuingia kunyakua.

Akitoa tathmini ya unyakuzi wa vipande vya ardhi vya DVS katika maeneo tofauti nchini, Mkurugenzi Mkuu Dkt Obadiah Njagi anasema karibu asilimia 80 ya shamba la makao makuu ya shirika hilo yaliyoko eneo la Kabete, kiungani mwa jiji la Nairobi, imenyakuliwa.

Dkt Njagi akitembeza wageni na wanahabari katika maabara mbalimbali ya DVS, ambazo zinakodolewa macho na hatari ya ardhi yake kunyakuliwa. PICHA/ SAMMY WAWERU

Ardhi jumla ya makao hayo ikiwa hekta (Ha) 2, 912 Dkt Nyagi anasema hekta 2, 300 ambazo zimesitiri afisi, taasisi ya mafunzo ya AHITI, makazi ya wafanyakazi, maabara ya utafiti, ikiwemo eneo maalum la kutengea mifugo wanaougua maradhi hatari kwa minajili ya kuifanyia ukaguzi na utafiti, zimenyakuliwa.

Kulingana na shirika hilo la huduma za mifugo, ardhi zake zimeathirika katika kila kona ya nchi.

“Kwa mfano, eneo la Ukunda, Kaunti ya Mombasa, kwa jumla ya ekari 260 ambazo DVS ilikabidhiwa na serikali ekari 5 pekee ndizo zimesalia,” Dkt Njagi anafichua.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na Ukunda, Kabete, Ngong, Machakos, Nakuru, Garissa na Maseno, Dkt Njagi akieleza kwamba mbali na wanyakuzi binafsi, taasisi zingine za serikali zimeingilia mashamba ya DVS bila kufuata sheria.

Mkurugenzi huyo Mkuu anasema shirika hilo linaendelea kupambana na kesi kadha mahakamani, baadhi likishinda ila halijarejeshewa vipande vilivyonyakuliwa kwa sababu walioshtakiwa hukata rufaa kortini.

Ramani ya ardhi ya makao makuu ya DVS eneo la Kabete. PICHA/ SAMMY WAWERU

Unyakuzi wa ardhi ya taasisi hiyo ya serikali ulianza mwaka wa 1985, baadhi ya wahusika wakisemekana kubomoa makazi yaliyokuwa yamejengwa.

DVS haijakabidhiwa hatimiliki ya mashamba yake mengi. “Hali ni mbaya kiasi kuwa tunalemewa kutoa huduma za mifugo nchini,” Dkt Njagi akalalamika wakati wa mahojiano, akiihimiza serikali kuingilia kati.

Taifa Leo Dijitali ilifanikiwa kupata na kukagua ramani ya ardhi ya shirika hilo, na unyakuzi ni wazi, baadhi ya wanaodaiwa kunyakua wakiweka ua na wengine ‘kuziboresha polepole kwa majengo’.

“Baadhi ya vipande vimenyakuliwa na kuuziwa watu binafsi, kampuni za kibinafsi, taasisi za serikali na makanisa, hatua ambayo imechangia unyakuzi kuvuka mipaka na vipande vingine kuingiliwa,” anafafanua Dkt Kiai Mwangi, Naibu Mkurugenzi Mkuu, na ambaye anashughulikia masuala ya ardhi na raslimali ya DVS.

“Ili DVS iweze kuendesha huduma zake, inahitaji ardhi. Unyakuzi ukiendelea tunavyoshuhudia hii leo, shirika hili litakuwa katika hatari. Mashamba ya taasisi hii yanapaswa kurejeshwa na kulindwa,” anasisitiza Dkt Kiai.

Ramani ya saveya inaonyesha kifungu 189R na 2952R, vya ardhi ya Kabete, awali vilitengewa hekta 1,634 na 1, 278, mtawalia.

Kwenye ziara ya Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya katika makao makuu ya DVS, alikiri kupokea malalamishi ya shirika hilo kuhusu unyakuzi wa ardhi.

Waziri wa Kilimo Bw Peter Munya alipozuru makao makuu ya Shirika la Mifugo Nchini (DVS), eneo la Kabete kiungani mwa jiji la Nairobi kuangazia kero ya unyakuzi wa ardhi wa taasisi hiyo ya serikali. PICHA/ SAMMY WAWERU

Waziri Munya hata hivyo alisema wizara yake inashirikiana kwa karibu na idara ya mashamba na taasisi zingine husika, kufichua ukweli na unyakuzi ulivyotekelezwa.

“Tutafanya ukaguzi na uchunguzi kujua idadi au ukubwa wa ardhi zilizosalia, ili tufahamu kiwango cha zilizonyakuliwa zirejeshwe,” Bw Munya akaahidi.

Vilevile, alisema ripoti ya ukaguzi itaeleza unyakuzi ulivyofanyika na ni kina nani walihusika kuutekeleza.

Huku kitendawili cha unyakuzi wa ardhi ya shirika hilo kikisalia gizani, DVS inanyooshea kidole cha lawama saveya aliyepewa au waliopewa jukumu kugawanya mashamba yake, ikihoji waliohusika walikiuka mkataba.

Huku maeneo mengi ya DVS yakiwa sehemu maalum za kutengea mifugo wenye magonjwa hatari na sugu, kwa minajili ya ukaguzi na utafiti wa kiini ili kupata tiba, shirika hilo linaonya kuwa unyakuzi wa ardhi yake unatia umma na mazingira katika hatari.

DVS inasema maradhi mengine yanayoshuhudiwa kwa mifugo yanaweza kuambukizwa binadamu.

Mbali na ardhi ya DVS kunyakuliwa, shirika hilo linalalamikia upungufu wa fedha na wafanyakazi kuendeleza huduma zake.

You can share this post!

Kituo cha Walibora hatarini kufifia baada ya kifo chake

AKILIMALI: Jinsi ufinyanzi inavyomfaidi