Habari Mseto

Shiviske Shivisi apania kufikia hadhi ya Viola Davis katika maigizo

April 7th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ANAJIVUNIA kuchota wafuasi wengi tu ndani ya miaka minne alipokuwa akishiriki kati ya vipindi maarufu hapa nchini ‘Tahidi High’ akifahamika kama Ayetsa ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.

Anasema amepania kujituma kiume ili kufikia hadhi ya mastaa mahiri katika tasnia ya uigizaji duniani kama Viola Davis.

Kutana naye Shiviske Shivisi anayedokeza kwamba tangu akiwa mtoto hakudhania angekuwa mwana maigizo. Kipusa huyu anajivunia kuwa mwigizaji, mwandikishi wa script pia prodyuza chipukizi wa kuzalisha filamu.

Mrembo huyu mwenye umri wa miaka 28 anasema alitamani kuhitimu kwa taaluma nyingi tu ikiwamo mtaalamu wa upasuaji.

”Pia nilitamani kuwa wakili bila kuweka katika kaburi la sahau kuwa mwalimu,” alisema na kuongeza kuwa ameamini Mungu ndiye anayefahamu maisha ya mwanadamu kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Anadokeza kuwa kimiujiza alianza kujituma katika masuala ya maigizo mwaka 2009. Alianza kufanya kazi na kundi la kundi la Fanaka Arts walipokuwa wakizalisha michezo ya kuigiza wakitumia mwongozo wa vitabu vya riwaya. Asilimia kubwa ya makundi hayo hutengeneza michezo ya kuigizaji ambayo huonyeshwa katika shule tofauti za sekondari nchini.

Kama mzalishaji filamu, anasema gharama kubwa inawalemaza wengi na kushindwa kutekeleza shughuli zao ipasavyo. Picha/ John Kimwere

Kando na Tahidi High, ameshiriki filamu nyingi tu ikiwamo Trade Centre ilionyeshwa kupitia Zuku, Bypass resort (Show max) na Nganya (Iflix) kati ya zingine. Kadhalika anajivunia kushiriki flamu kama Ashiki chini ya kundi la Spielworks Media pia Poacher (QBF) miongoni mwa zingine.

Mwaka jana alizalisha filamu fupi ‘My Jubilee’ iliyoteuliwa kwenye tuzo za ‘Smart Phone Short Film’ zilizoandaliwa na Alliance Francaise. Filamu hiyo ilifanikiwa kutwaa tuzo hiyo kitengo cha filamu mpya (New Comer).

Anasema serikali inapaswa kuamini kazi za waigizaji wa humu nchini na kuwekeza katika sekta ya maigizo ili kusaidia wasanii chipukizi.

Anashikilia kwamba serikali inastahili kupunguza ada ambayo hutoza kampuni za kuzalisha filamu wakati wa kurekodi kazi zao ili kuvutia wawakezaji wa kigeni kufanya shughuli zao hapa nchini.

”Ada ya juu imechangia serikali kupoteza fedha nyingi na kudidimiza uchumi wa taifa hili,” alisema na kutoa mwito kwa wambunge wa bunge la kitaifa kuwazia suala hili kwenye juhudi za kuinua sekta ya maigizo nchini.

Kadhalika anazitaka serikali za Kaunti kutilia maanani tasnia ya maigizo ili kubuni ajira kwa wasanii chipukizi. Pia anasema analenga kujitahidi awezavyo kuhakikisha ametimiza ndoto ya kumiliki kampuni ya kuzalisha filamu miaka ijayo. Anadokeza kuwa amepania kuanzisha kampuni yake ili kusaidia waigizaji chipukizi nchini.

Demu huyu amepitia changamoto gani? Anasema makundi mengine huchelewesha malipo ya wasanii na kuwafanya kujikuta kwenye wakati mgumu hasa kugharamia mahitaji muhimu katika maisha ya mwanadamu.