Shofco Mathare yaota mizizi ikilenga kupanda daraja

Shofco Mathare yaota mizizi ikilenga kupanda daraja

NA JOHN KIMWERE

NI miongoni mwa vikosi vinavyotifua vumbi kali kwenye kampeni za ngarambe ya kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu.

Licha ya kuwa inashiriki ngarambe hiyo kwa mara ya kwanza, Shofco Mathare inaendelea kufanya vizuri kwenye kampeni hizo huku ikilenga kuibuka kileleni na kujikatia tiketi ya kushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu ujao.

”Shofco Mathare FC ni kati ya timu zinazowazia kushiriki mechi za kuwania taji la Mashirikisho Soka la Afrika (CAF) miaka ijayo,” kinara wa kituo cha Shofco Mathare, Godfrey Waka alisema na kupongeza kuwa wachezaji wa kikosi hicho kwa kujituma kwao kwenye michuano ya muhula huu.

Afisa huyo anasema kuwa wachana nyavu wake wanafanya kazi nzuri ingawa wanakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wao.

Shofco Mathare FC ilisajili wachezaji wapya 11 mwanzoni mwa muhula huu ilipopandishwa ngazi ili kuchochea wenzao kwenye kampeni za kipute hicho.

Kocha mkuu, Fahzul Ongoya Joshua anasema ana wachezaji wazuri wenye uwezo wa kufanya kweli kwenye kampeni za msimu huu. ”Nikitazama wachezaji wangu sina shaka kutaja kuwa wakiendeleza kasi yao pia waendelee kutuchezea tunajipatia miaka mitano pekee kuhakikisha tumetinga kushiriki soka la hadhi ya juu nchini,” alisema.

Kwenye shughuli za kusukuma gurudumu la timu hii kocha huyo husaidiana na kocha Leakey Agufa, Dominic Omondi (meneja) na daktari Lavender Akoth.

”Kando na malengo ya kushiriki soka la hadhi ya juu miaka ijayo pia tumepania kunoa makucha ya wachezaji wengi tu na kufanikiwa kuchezea vikosi vya ligi mbali mbali nchini pia kimataifa,” kocha Leakey Agufa alisema na kuongeza kuwa fani hiyo imeibuka kitengo uchumi kwa wanasoka wengi duniani wanaume na wanawake.

Hata hivyo anadokeza kuwa wanaohofia pakubwa wapinzani wao ikiwamo Kasi kasi FC, Karura Greens, Mainstream Academy FC, Maroons Young Stars na Red Carpet FC kati ya nyingine.

Anashikilia kuwa vikosi hivyo vinakuja kwa kasi kwenye kampeni za muhula huu ambapo wakiteleza tu watapigwa breki.

Shofco Mathare inajivunia kukuza wachezaji kadhaa na kujiunga na klabu nyingine.

Orodha ya wachana nyavu hao inajumuisha: Felix Omondi, Dennis Osinya, Paul Odhiambo na Brian Ochieng.

Kocha mkuu anashukuru kituo cha Shofco kwa kufadhili kikosi hicho kwenye jitihada za kukuza wachezaji wanaokuja.

”Ni furaha kwa wanasoka chipukizi kupata nafasi kunoa makucha yao huku wakilenga kutinga hadhi ya wanasoka wa kimataifa miaka ijayo,” akasema.

Kadhalika anashauri kocha klabu za Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF-PL) washuke mashinani kusaka chipukizi wenye talanta.

Timu ya Shofco Mathare FC. PICHA | JOHN KIMWERE

Shofco Mathare FC iliasisiwa miaka 2014 na hupatikana eneo la Mathare Area B ambapo mechi za nyumbani huchezea kwenye uwanja wa Mathare Area4, Police Depot. Klabu hii inajivunia kushinda mataji manne tangia ianzishwe.

Shofco Mathare FC inashirikisha: Michael Misolo, Philip Mwendwa (nahodha), Dereck Otieno, Paul Odhiambo, Julius Were(naibu wa nahodha), Dennis Osinya, Brian Ochieng, Enock Muuwo (naibu wa nahodha), Dennis Otieno, Helmut Omondi, Vincent Nzomo, Mark Raphael, Michael Odida, Shadrack Omondi, Antony Onyango, Philip Kalika, Lenox Okello na Analo Daniel. Pia wapo Brian Otieno, Denis Akello, Evans Adoma, Badii Miheli, Levy Onyango, Michael Omondi, Stephen Ochieng, Vincent Ouma, Victor Odwour, Vincent Masime, Obina Wisdom, Felix Omondi na Henry Ouma.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wachunguza Mbogo kwa madai ya uchochezi

PAUKWA: Bikizee akumbana na kudura ya Mungu

T L