Habari Mseto

Shoka kuwaangukia waasi wa mrengo wa Nasa katika bunge la kitaifa

May 27th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kiminini Chris Wamalwa na mwenzake wa Malindi Aisha Jumwa watakoponywa nyadhifa za naibu kiranja wa wachache na kamishna wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) katika mabadiliko yatakayotekelezwa na mrengo wa Nasa.

Akiongea na wanahabari Jumatano jijini Nairobi, kiranja wa wachache Junet Mohamed alisema vyama tanzu katika muungano huo vimeitisha mkutano wa Kundi la Wabunge Alhamisi ambapo atawasilisha orodha ya wawili hao na wabunge wengine waasi.

Wabunge wengine saba watakaopoteza nafasi zao katika kamati mbalimbali za bunge la kitaifa ni pamoja na Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini, KNC), Tindi Mwale (Butere, ANC), Gideon Ochanga (Bondo), Nakara Lodepe (Turkana ya Kati, ODM), Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi, Ford Kenya) na Catherine Mwambilianga (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Bungoma, Ford Kenya).

“Wabunge hawa tunawaondoa kwa sababu wamedhihirisha kwamba sio waaminifu kwa sera na mwongozo wa muungano wa Nasa. Baadhi yao wamekuwa wakikwepa kuhudhuria vikao vya kamati wakitumia muda wao mwingine kuzunguka mijini bila sababu maalum,” akaeleza Bw Mohamed ambaye pia ni mbunge wa Suna Mashariki.

Hatua hii inajiri siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju kuthibitisha kuwa chama hicho kitawatimua wabunge wake kadhaa wanaoshikilia nyadhifa za uongozi katika bunge la kitaifa.

Duru zinasema kuwa wanaolengwa ni kiongozi wa wengi Aden Duale, kiranja wa wengi Benjamin Washiali, naibu wake Cecily Mbarire, mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu bajeti Kimani Ichung’wah miongoni mwa wengine.

Wiki jana Jubilee ilitekeleza mageuzi kwa uongozi wake katika Seneti kwa kumpokonya Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen wadhifa wa kiongozi wa wengi.

Seneta wa Kaunti ya Nakuru Susan Kihika na mwenzake wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki pia walivuliwa nyadhifa za kiranja wa wengi na naibu spika, mtawalia.