Habari MsetoSiasa

Shoka la Obado latia hofu maafisa wakuu

November 1st, 2018 1 min read

Na ELISHA OTIENO

HOFU imekumba maafisa wakuu katika Kaunti ya Migori baada ya Gavana Okoth Obado kuanza kufanya mabadiliko katika serikali yake.

Maafisa wengi wanalengwa kusimamishwa kazi kwa madai ya kutokuwa waaminifu kwa gavana huyo aliyerejea kazini baada ya kukaa rumande kwa mwezi mmoja kuhusiana na mauaji ya aliyekuwa mpenzi wake, Bi Sharon Otieno.

Imedaiwa kuna maafisa wengi wamekuwa wakijifanya kutekeleza matakwa ya Bw Obado ilhali wana malengo ya kujinufaisha kibinafsi.

Bw Obado ambaye anatumikia awamu yake ya pili na ya mwisho ameamua kufanya mabadiliko hayo bila kujali athari zitakazotokea kwake kisiasa, kwa mujibu wa mmoja wa wandani wake aliyeomba asitajwe.

“Kuna watu ambao watalazimika kujiuzulu kwani wakati huu hakuna huruma kwa yeyote,” akasema. Yamkini, uamuzi wa gavana huyo ulishika kasi alipokaa rumande Industrial Area jijini Nairobi kwa zaidi ya siku 30.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh5 milioni pesa taslimu na wadhamini wawili wa kiasi sawa na hicho, mbali na kuwekewa masharti makali yanayomzuia kutoka nje ya Migori. Duru zilisema sasa lengo lake ni kuacha sifa ya uongozi bora katika kaunti hiyo.

“Hii ndiyo maana wanafiki lazima waondoke upesi. Gavana atakuwa na msimamo mkali wakati huu ikilinganishwa na ilivyokuwa katika muhula wake wa kwanza,” akasema msaidizi huyo.

Gavana huyo tayari alianza kuhamisha baadhi ya maafisa wake na inaaminika shughuli hii itaendelea kwa majuma kadhaa yajayo.