Makala

Shollei atwikwa hadhi ya juu katika jamii ya Agikuyu

March 3rd, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

WAKATI mwanasiasa Gladys Jepkosgei Boss Shollei, mbunge mwakilishi wa Kaunti ya Uasin Gishu alipotwikwa hadhi ya Nyakinyua na jamii ya Agikuyu inayoishi katika Kaunti ya Uasin Gishu iliashiria kuwa amekomaa kirika.

Bi Shollei ambaye ni wakili kitaaluma na aliyehudumu kama msajili wa mahakama kuu na ambaye pia ni mwandani wa Rais William Ruto kwa sasa amekumbatiwa kama mwanamke wa jamii ya Agikuyu

Taji hilo la “Nyakinyua” ni la saba katika viwango vya maisha ya mtoto wa kike katika jamii ya Agikuyu ambapo huanza na kuwa “Kaana”, kumaanisha mtoto kisha anatinga umri wa kuitwa “Karigu” ambaye ni msichana mdogo ambaye bado hajapashwa tohara.

Lakini mila hii ya kupasha wasichana tohara katika jamii hiyo imeorodheshwa rasmi kimila na kisheria kama iliyopitwa na wakati na ukinaswa ukiishiriki, unashtakiwa.

Awamu ya tatu ni ile ya “Muiritu” ambaye aliwekwa katika umri wa baada ya tohara lakini akiwa bado hajaoelewa.

Kiwango che nne ni kile cha “Muhiki” ambaye yuko ndani ya mwaka wa kwanza baada ya kuolewa na akipata mtoto wa kwanza anaingia katika ile awamu ya tano ambayo akiwa ni mama wa mtoto wa kwanza anaitwa “Muhiki wa rwara rumwe” (msichana wa kucha moja).

Katika awamu ya sita ni “Mutumia wa Kang’ei” ambaye sasa anakubalika kama aliyekomaa kimaisha na ndani ya ndoa na ambaye hata anaweza akajitosa ulingoni mwa densi katika ndoa ya wengine kunengua kiuno na hata kushiriki hafla kuwasilisha mahari.

Hata hivyo, viwango hivi vya kimila viliashiria maisha ya mwanamke akiwa atafuata utaratibu wote hadi kuingia kwa ndoa, lakini katika dunia ya sasa ambapo wanawake wengi wamesusia au wameikosa ndoa, hali imeishia kuvurugika na kuyeyuliwa kabisa na upenyo wa itikadi za kisasa.

Awamu ya saba sasa ambayo Bi Shollei amekubalika kuwa katika jamii hiyo ni “Mutumia wa Nyakinyua” ambaye kigezo ni kuwa na watoto wasiopungua watatu wa jinsia yoyote na ambao wametinga umri wa kupashwa tohara, hadhi kuu kwake ikiwa yuko huru kunywa pombe lakini kwa ustaarabu na nidhamu kuu asiharibu mambo.

Kuna awamu ya nane na ambayo ni tata ambayo inaitwa “Mutumia wa makanga” ambayo ni kuhusu mwanamke ambaye amepitisha uwezo wa kuzaa watoto lakini bado angali mtaani akikimbizana na ngono. Jina hilo ametwikwa kuwa sawa na gari katika steji ambalo hung’ang’aniwa na makanga libebe abiria.

Awamu ya mwisho huwa ni Kiheti ikimaanisha mwanamke mkongwe ambaye hana uwezo wa kujitoa nyumbani kushiriki maisha kamili ya mtoto msichana wa jamii hiyo.

Mwenyekiti wa baraza la jamii ya Agikuyu Bw Wachira Kiago alisema chini ya mila za jamii hiyo mgeni anaweza akakaribishwa na atuzwe baada ya kukadiriwa kuwa rafiki wa kuletea jamii hiyo faida za amani na ustawi.

Mama wa watoto watano, Bi Shollei alitalikiana na bwanake Bw Sam Shollei mwaka wa 2021 lakini akakubali hali na akaoga, akarejea sokoni na chini ya miaka mitatu akanasa wake tena wa roho.