HabariSiasa

Shollei motoni kwa kutopigia debe Ruto

April 23rd, 2019 1 min read

DENNIS LUBANGA na WYCLIFF KIPSANG

TOFAUTI kali za kisiasa zimezuka kati ya Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Uasin Gishu, Gladys Shollei na viongozi wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, kwani amekuwa akikwepa kuhudhuria hafla zake.

Kinyume na viongozi wengine wa kisiasa katika eneo hilo, Bi Shollei amekuwa akiendesha shughuli zake kichinichini bila kuwahusisha.

Hilo limemfanya kukosolewa pakubwa na viongozi wanaomuunga mkono Dkt Ruto. Hata hivyo, Bi Shollei, ambaye alichaguliwa kwa tiketi Chama cha Jubilee (JP), alisisitiza kuwa atakuwa akiendesha shughuli zake bila kuzingatia mawimbi ya kisiasa.

“Mimi ni kiongozi tofauti anayeendesha majukumu yake kwa njia huru. Simtegemei kiongozi yeyote wa kisiasa ili kujipa umaarufu,” akasema, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

“Ninawaheshimu viongozi wote, wakiwemo walio katika Uasin Gishu. Hata hivyo, sitakuwa nikihudhuria mikutano ya kisiasa bila ajenda zozote. Sitakuwa nikipoteza muda wangu,” akasema.

Alisema kwamba atakuwa akiendesha shughuli zake kwa njia huru na ‘hatajiuza’ ili kuwafurahisha watu kwa lengo la kuchaguliwa tena.

Jumapili iliyopita, Bi Shollei alijipata pabaya baada ya kupigiwa kelele na baadhi ya wakazi alipotoa hotuba wakati wa Mbio za Riadha za Eldoret.

Kwenye hotuba yake, Bi Shollei alijitenga na makundi ya ‘Kieleweke’, ‘Tanga Tanga’ na wale wanaounga mkono muafaka wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga. “Hutaniona katika hafla za makundi ya ‘Tanga Tanga’ au ‘Kieleweke.’

Hii ni kwa kuwa naamini katika maendeleo badala ya siasa. Sitakuwa nikiandamana nao,”akasema.

Hata hivyo, alionekana kutobabaishwa na kelele hizo, akisisitiza kwamba hatajitosa katika siasa.

Ilibidi Naibu Gavana Daniel Chemno kuingilia kati ili kuutuliza umati huo.

Bi Shollei, ambaye alihudumu kama Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama hajakuwa akiandamana na kundi la ‘Tanga Tanga’ licha ya kuchaguliwa kwa tiketi ya Jubilee.