Dondoo

Shuga mami atupa polo nje kugundua ana mwingine

September 15th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KABETE, KIAMBU

Polo mmoja alijipata akihangaika mtaani hapa baada ya kutimuliwa na shuga mami kwa kukaidi makubaliano yao.

Inasemekana tukio hili lilitokea baada ya shuga mama kugundua kwamba polo ana mpenzi mwingine kinyume na makubaliano yao.

Kulingana na mdokezi, mama huyo alikuwa akiishi na polo kwa makubaliano kuwa polo hatawahi kutafuta mrembo mwingine.

Duru zinasema bosslady alikuwa akimpa polo kila kitu alichokuwa akihitaji. Kwa upande wake, polo naye alifaa kumtimizia shuga mama mahitaji fulani.

Penyenye zinasema mambo yalimharibikia polo shuga mami alipopata fununu kuwa polo alikuwa na mchumba mwingine kisiri.

“Juzi ulipotoka hapa ulienda wapi?” alimuuliza jamaa ambaye alishindwa la kusema. Shuga mami alisimama na kuanza kumfokea.

“Mimi sipendi watu ambao wana uongo. Kwa hii nyumba yangu nakupa kila kitu. Ni nini unakosa hapa?” shuga mama alimfokea polo.

Inadaiwa polo alijitetea kwa kumuambia alikuwa ameenda kumuona rafiki yake fulani.

“Rafiki gani huyo ambaye hutaki kuniambia nimjue. Sitaki mambo yako tena. Tembea,” mama alimkaripia polo. Duru zinasema polo alibaki mdomo wazi. Alishindwa aanzie wapi.

“Ulipokuja kwangu ulikuwa na shati moja na suruali mbili. Zichukue na uanze safari,” jamaa alishurutishwa.

Inasemekana jamaa aliomba msamaha kwa kupiga magoti lakini hakutoboa. “Nimesema enda kwa yule mrembo wako. Kwangu nimekupa likizo. Sipendi watu wasioridhika na mimi. Nitatafuta mwingine achukue nafasi yako,” shuga mama alimfokea polo.

Kulingana na mdokezi, kipusa aliingia chumbani na kumrushia polo nguo zake.

“Mpelekee yule mrembo wako akuoshee. Kwangu usikanyage tena,” mama huyo alimuonya polo.