Dondoo

Shugamami atimua polo kutesa familia

September 5th, 2019 1 min read

NA NICHOLAS CHERUIYOT

KERICHO MJINI

MAMASUKARI wa eneo hili, alimfurusha barobaro kwake alipogundua kwamba kijana huyo aliacha mke na watoto wakihangaika.

Kulingana na mdokezi, shuga mami alimpata jamaa mjini na mara moja akamfanya kuwa mtu wa kumpasha moto mara kwa mara.

“Mama alimwagia jamaa hela na maisha ya polo yakabadilika ghafla naye akijikaza kutimiza majukumu yake,” mdaku akeleza.

Marafiki wa mama huyo walimkosoa wakimwambia huenda anavunja boma la jamaa huyo lakini mama alijitetea vilivyo.

“Mimi siwezi kumharibia kijana maisha. Ukweli ni kwamba alinieleza kuwa alibaki na mahangaiko bwanyenye mmoja alipomnyakua mkewe na kumtumbukiza kwenye upweke wa kipekee ndipo akahamia mji huu kusaka unga na kujiokoa asije akajinyonga huko ushago,” mama alisema kisha akawataka wenzake wacheze mbali wamuache aponde raha kama wanawake wengine.

Hata hivyo, wenzake walimtaka achunguze vizuri barobaro huyo badala ya kukubali tu maelezo ya polo.

Mama alianza uchunguzi wa kina na baada ya muda mfupi ukweli ukabainika.

“Duru zilizoaminiwa na mama zilimwarifu kuwa jamaa alikuwa amemtelekeza mke na watoto wakazama kwenye lindi la umaskini,” mdaku aliarifu.

Hofu ilimpanda mama alipodokezwa kuwa mkewe wa alikuwa akipanga safari hadi mjini akiandamana na watoto kumlilia amwachilie huru jamaa huyo.

Jioni ya siku hiyo, jamaa aliyumbayumba kuelekea kwa shugamami akitoka mangweni lakini alipofika alikemewa vilivyo na mwenyeji wake.

“Ingia ndani utoe mali na uende uokoe jahazi huko ushago. Hauwezi kufurahia hela zangu huku watoto wako wakiombaomba kijijini,” mama alimweleza jamaa.