Makala

SHUGHULI: Aliacha udereva akaanza upakaji rangi

November 28th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

YAPATA miaka saba imepita tangu Bw Paul Muli aache kazi ya kuajiririwa ili kujiajiri binafsi.

Alikuwa dereva wa kampuni moja ya kibinafsi, na kulingana na simulizi yake wakati huo asingeweza kuweka akiba yoyote kwa sababu ya gharama ya mahitaji.

“Mapato yalikuwa haba yakilinganishwa na mahitaji ya familia yangu,” anasema Bw Muli ambaye ni baba ya watoto watatu.

Hata hivyo, alichukua hatua nyingine; kutathmini kuhusu maisha ya usoni, akaamua kuingilia sekta ya juakali, anayoitaja kama yenye mapato ya kuridhisha.

Bw Muli hufanya kazi ya kupaka rangi kwenye majengo au majumba na uandikaji wa majina au maandishi kutani na kwenye mabango.

“Hii ni kazi ya juakali, ya kujiajiri na ina mapato ya kuridhisha nikiilinganisha na niliyoifanya awali,” anafafanua akiisifia.

Isitoshe, ni kazi ya sanaa inayohusisha uchoraji.

“Haina presha wala msukumo wowote kuifanya kwa sababu mimi ndiye bosi,” anaongeza.

Aidha, juakali inaorodheshwa katika sekta ya biashara ndogondogo na zile za wastani (SMEs), ambazo zinakadiriwa kuwakilisha zaidi ya asilimia 75 ya nguvukazi nchini.

Kimsingi, inaongoza katika ubunifu wa ajira Kenya.

Muli anasema amejaaliwa talanta ya uchoraji, ikizingatiwa kuwa alifanya mtaala wa 8- 4 -4, mfumo wa elimu ambao umekuwepo nchini kwa zaidi ya miaka 20.

Mfumo huo ulijumuisha Somo la Uchoraji, Sanaa na Ususi pia Ufumaji maarufu kama Art & Craft, kwa mujibu wa walioufanya. Pia ulikuza vipaji kama vile waliojaaliwa uimbaji, kupitia vipindi vya nyimbo.

Pauli Muli anaambia Taifa Leo kwamba vipindi vya Art & Craft vilimnoa na kumuimarisha kisanaa; uchoraji. Ni kupitia kipaji hicho 2011 baada ya kuacha kazi ya udereva aliamua kukifufua.

Anasema ilimgharimu mtaji wa Sh5, 000 pekee. “Nilitumia pesa hizo kununua vifaa kama vile breshi,” aeleza Muli.

Kwa chipukizi, zana za kazi ni muhimu na kuwa na wa kumuongoza. Muli anafichua kwamba akiwa dereva alikuwa akifanya kazi hiyo kama gange ya ziada, ili kupiga jeki mapato yake, hivyo basi alikuwa na wateja waliomtambua.

Gharama ya rangi ni kwa mteja; anayetaka kupakiwa jengo rangi, au kufanyiwa maandishi kwenye majengo au mabango.

Msanii huyo anasema leba huambatana na kiwango cha kazi pamoja na maelewano.

“Kuna majengo ninayotoza hata zaidi ya Sh50, 000, pia ninaajiri vijana wa kunisaidia kufanikisha majukumu niliyotwikwa,” anasema.

Hata hivyo, anasema gange ya upakaji rangi na uchoraji inahitaji umakinifu wa hali ya juu, hususan katika kuchanganya rangi mbalimbali ili kuibuka na anavyotaka mteja.

Kauli yake inatiliwa mkazo na Edward Gikaria, maarufu kama Eduardo wa Brush mtaani eneo la Githurai, ambaye ni gwiji katika shughuli za upakaji rangi.

“Ukikosea kuchanganya rangi, utakuwa umesababisha hasara na utaigharamia mwenyewe ili kuafikia matakwa ya mteja,” anasema Bw Gikaria.

Wakati wa mahojiano na Paul Muli tulipompata akiwa katika harakati za kuandika majina kwenye ukuta wa kanisa moja eneo la Mumbi, Kaunti ya Kiambu, alisema si mara moja au mbili amelazimika kugharamia kosa la uchanganyaji rangi isivyofaa.

“Kuna rangi zinazochanganywa ili kupata nyingine. Inahitaji umakinifu, na kutambua uhalisia wa rangi,” Bw Muli akasema.

Maeneo anayolenga ni yenye shughuli za ujenzi wa majengo ya makazi, shule na pia hupata kandarasi za kampuni au mashirika. Pia hufanya maandishi ya malango na mabango.