Habari Mseto

Shughuli nyingi zinazoisubiri Bunge kuanzia Februari 12

February 5th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa linarejelea vikao vyake mnamo Februari 12, 2019 baada ya likizo ndefu ya Krismasi na Mwaka Mpya huku likikabiliwa na shughuli nyingi ikiwemo kupiga msasa atakayechukua mahala pa Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet anayestaafu.

Kipindi cha kuhudumu cha Bw Boinnet kinakamilika mnamo Machi mwaka huu na kumekuwa na mjadala kuhusu ni nani atapewa wadhifa huo wenye ushawishi mkubwa katika sekta ya usalama.

Boinnet aliteuliwa mnamo Desemba 2014 kuchukua mahala pa Bw David Kimaiyo aliondolewa baada ya kuonekana kulemewa na majukumu.

Kiongozi wa wengi Aden Duale pia alisema bunge litashughulikia tena mswada kuhusu uwepo wa usawa wa jinsia katika asasa za uongozi, baada ya shughuli hiyo kuahirishwa mwishoni mwaka jana kutokana na uhaba wa idadi tosha ya wabunge.

Mswada huo unalenga kuhakikisha kuwa angalau thuluthi moja ya wabunge na maseneta ni wa jinsia tofauti. Mswada huo unahitaji kuungwa mkono na angalau wabunge 233 katika awamu ya pili lakini mnamo Desemba 6, 2018 siku ambayo ingepigiwa kura ni wabunge 216 walikuwa ukumbini hali ilimpelekea Bw Duale kuomba shughuli hiyo iahirishwe.

Kuhusu uteuzi wa Inspekta Jenerali mpya, Bw Duale alisema Alhamisi kwamba baada ya kupokea jina mtu aliyependekezwa na Rais pamoja na Tume ya Kitaifa ya Polisi (NPSC), kamati husika itampiga msasa kabla ya kumwidhinisha au kumkataa.

“Bunge litakaporelea mnamo Jumanne Fabruari 12, ajenda ya kwanza itakuwa ni mjadala wa kuhusu mswada wa usawa wa jinsia,” akasema Bw Duale huku akielezea matumaini kuwa wabunge watapitisha mswada huo wakati huu.

“Baada ya kujua siku ambayo mswada huo utapigiwa kura, wabunge wa mirengo ya Jubilee na NASA watakutana na kushawishi wanachama wao kuhudhuria bunge kwa wingi. Wakati huu tuna imani kuwa zaidi ya wabunge 233 watafika bungeni kuupigia kura mswada huo,” mbunge huyo wa Garissa Mjini akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

Baada ya mswada huo kupitishwa katika awamu ya pili, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ataiwasilisha kwa awamu ya tatu, maarufu kama Kamati ya Bunge lote ili upigwe msasa zaidi kabla ya kupitishwa katika kikao kitakachotengwa.

Wakati huu, Bunge la Kitaifa lina wabunge wanawake 76. Na kati ya hao, 23 wamechaguliwa kutoka maeneo bunge, 47 wanawakisha kaunti na sita ni wabunge maalum.

Katika bunge la Seneti kuna wanawake 21 ambapo 19 kati yao wameteuliwa na vyama huku watatu ni wale wamechaguliwa. Waliochaguliwa ni Bi Fatuma Dullo (Isiolo), Profesa Margaret Kamar (Uasin Gishu) na Susan Kihika (Nakuru).

Wakati huo huo, Bw Duale alisema bunge pia litashughulikia utayarishaji wa bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2010.