Habari Mseto

Shughuli ya kuwapiga msasa polisi wa akiba itaimarisha utendakazi wao – Ruto

June 8th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amesema Jumamosi serikali inaendelea na mpango wa kukifanyia marekebisho kitengo cha polisi wa akiba (NPRs) kwa lengo la kukiboresha kwa minajili ya kuimarisha usalama katika maeneo kame na yaliyotengwa kimaendeleo.

Akiongea katika kaunti ya Samburu Dkt Ruto alisema mpango wa kuwapiga msasa polisi hao wa akiba utaendeshwa kwa ushirikiano na viongozi wa maeneo husika.

“Ni wajibu wa serikali kutoa usalama kwa wakazi wa maeneo yaliyotengwa. Hii ndio maana tunawarekebisha polisi wa akiba ili kuimarisha utendakazi wao. Na viongozi wenu hapa wanashirikishwa katika mpango huo,” akasema.

Kaunti ya Samburu ni mojawapo ambayo imeshuhudia ongezeko la visa vya utovu wa usalama katika siku za hivi karibuni baada ya serikali kuwapokonya NPRs bunduki.

Shughuli hiyo pia iliendeshwa katika kaunti za Laikipia, Turkana, Elgeyo Marakwet, Baringo na Isiolo na Pokot Magharibi.

Wizi wa mifugo

Viongozi kutoka maeneo hayo walilalamikia hatua hiyo wakisema ndiyo imechangia ongezeko la visa vya wizi wa mifugo na ujangilia katika kaunti hizo kwani wahuni bado wanamiliki silaha haramu.

Baadhi ya viongozi hao ni magavana John Lonyangapuo (Pokot Magharibi), Josephat Nanok (Turkana), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet), Nderitu Muriithi (Laikipia) pamoja na wabunge na maseneta kutoka maeneo hayo.

Wiki iliyopita Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen aliingiza siasa katika suala hilo kwa kudai kupokonywa bunduki kwa polisi hao wa akiba ni njama ya kuyeyusha umaarufu wa Dkt Ruto ili kuzima ndoto yake ya kuingia Ikulu.