Michezo

Shughuli ya uteuzi wa timu ya Olimpiki kukamilika Juni 2020

November 6th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KENYA itawakilishwa na takriban wanaspoti 80 katika Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan.

Idadi hiyo ni nyongeza ya wanamichezo 13 zaidi, kutoka 67 waliopeperusha bendera ya taifa kwenye Olimpiki za 2016 zilizofanyika jijini Rio, Brazil.

Olimpiki za 2020 jijini Tokyo zitafanyika kati ya Julai 24 na Agosti 9 mwaka ujao.

Msimamizi wa kikosi cha Kenya katika michezo hiyo, Bw Waithaka Kioni, alisema kuwa wanaspoti 45 wa humu nchini tayari wamefuzu kwa mashindano hayo. Hao ni pamoja na waogeleaji wawili, wanariadha 28 na wanaraga wa timu ya taifa ya wanawake, Kenya Lionesses.

Vikosi vingine vinavyotarajiwa kufuzu ni timu ya taifa ya soka ya wanawake (Harambee Starlets), timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande kwa wanaume (Shujaa), timu ya taifa ya voliboli ya wanawake (Malkia Strikers), timu ya taifa ya wanabondia na baadhi ya wanariadha ambao uteuzi wao unatazamiwa kukamilika Juni 2020.

Ikisalia miezi 10 pekee kwa mashindano ya Olimpiki kuanza, vinara wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC-K) wamekiri kuwa na kibarua kigumu.

“Licha ya changamoto mbalimbali zinazotukabili, tunaelekeza macho kwa Michezo ya Tokyo, Japan, mwakani.

“Tunashauriana na mashirikisho husika ili kukamilisha mchakato wa kuteua wanamichezo bora watakaowakilisha taifa na kutuletea tija na fahari tele,” akasema Kioni katika taarifa.

“Japo Nock itakuwa na jukumu la kutoa jezi kwa wote watakaoshiriki michezo hiyo, kila shirikisho litafadhiliwa na Wizara ya Michezo kufanikisha mipango ya kufuzu kwa wanaspoti wao,” akasema Mwekahazina wa Nock, Bw Eliud Kariuki, hapo Jumanne.

Vipimo vya afya

Wakati huo huo, vinara wa Nock wamesisitiza kwamba wanariadha wote watakaoteuliwa kuwakilisha Kenya jijini Tokyo watafanyiwa vipimo mbalimbali vya afya, ili kubaini iwapo wamewahi kutumia dawa za kusisimua misuli.

Kikosi cha Kenya nchini Japan kitakuwa chini ya meneja Barnabas Korir ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Tawi la Nairobi. Humphrey Kayange na Ahmed Swahib watakuwa manaibu wa Kioni.

Timu ya Kenya inatarajiwa kupiga kambi ya mazoezi mjini Kurume, Japan.