Shughuli zarejea kawaida baada ya shule iliyogeuza madarasa kuwa nyumba za kukodi kufunguliwa

Shughuli zarejea kawaida baada ya shule iliyogeuza madarasa kuwa nyumba za kukodi kufunguliwa

Na SAMMY KIMATU

SHULE moja ya mmiliki binafsi katika kaunti ya Nairobi ambayo ilikuwa imebadilishwa kuwa nyumba za kukodi imefunguliwa.

Aidha, Shule ya The Rock Academy iliyoko katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina katika kaunti ndogo ya Starehe, kama shule zingine kote nchini ilifungwa mnamo Machi 2020.

Hatua ya kufunga shule, vyuo vikuu na taasisi zote za elimu nchini ilifikiwa na serikali kufuatia janga la Covid-19.

Baada ya kugundua kuwa alikuwa akipata hasara kubwa kufuatia kufungwa kwa shule hiyo, mmiliki wa shule ya The Rock, Bi Christine Kathukya alisema aliamua kugeuza madarasa ya shule kuwa nyumba za kupangisha.

Juu ya lango kuu ukutani palitundikwa kibao na maandishi “Nyumba za kukodisha hapa.”

“Badala ya madarasa kukaa bila kazi huku mwenye nyumba bado alikuwa akinilipisha kodi, nilikuja na wazo la kukodisha watu nyumba katika darasa za shule yangu,” Bi Christine Kathukya aliambia Taifa Leo.

Bi Kathukya aliongeza kuwa licha ya janga la korona kuvuruga uchumi na shule nyingi za wamiliki binafsi kufungwa kabisa hatajuta kwani wazo lake lilizaa matunda.

“Fedha za nyumba zilizolipwa na wapangaji ziliniwezesha kupunguza gharama ya matumizi kama vile kuwalipa walimu na wafanyakazi wengine sawa na kumlipa mwenye nyumba pia,” Bi Kathukya alisema.

Kwa muhtasari, kodi ya nyumba ya jengo la mawe katika maeneo ya Hazina hugharimu kati ya Sh5,000 na Sh7,000 kwa kila chumba.

“Kodi ya nyumba zilizojengwa kwa mabati hugharimu kati ya Sh2,500 na Sh3,500 pamoja na choo na umeme,” Bw Mohammed aSoba Kutuni, mwenyekiti usalama mtaani akasema.

Jana, wanafunzi na walimu walikuwa na shughuli za kuendelea na masomo yao darasani kama hapo awali katika shule ya The Rock.

  • Tags

You can share this post!

Morocco wapepeta Mali na kuhifadhi ubingwa wa taji la CHAN

Mbwa apima corona kwa ufanisi mkuu