Michezo

Shuja wajiandaa kwa duru ya London

May 23rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya, almaarufu Shujaa, imeimarisha mazoezi yake kabla ya kuanza kampeni ya kutafuta alama kwenye duru ya London nchini Uingereza mnamo Mei 25-26 ili kujiondolea presha ya kutemwa.

Vijana wa kocha Paul Murunga wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama 26, alama nne pekee kutoka nafasi ya 15 ambayo mshikilizi wake Japan inakodolea macho kushushwa ngazi

Kenya itavaana na Fiji (12.36pm), Samoa (3.20pm) na Ufaransa (6.26pm) katika siku ya kwanza hapo Mei 25 kwenye mechi za Kundi B.

Shujaa ina ushindi mmoja katika mechi tano zilizopita dhidi ya nambari mbili Fiji uliopatikana jijini Paris nchini Ufaransa mnamo Juni 9, 2018. Imepoteza mechi nne mfululizo ikiwemo kulimwa 22-5 na wanavisiwa wa Fiji zilipokutana mara ya mwisho mjini Hong Kong hapo Aprili 5, 2019. Itakuwa ina kibarua kigumu kwa sababu imeshinda Fiji mara tatu pekee na kupepetwa mara 24 tangu mwaka 2011.

Vilevile, kibarua kigumu kinasubiri Shujaa dhidi ya Samoa. Shujaa ina ushindi 10 na kupoteza mara 14 katika mechi zake 24 zilizopita dhidi ya Samoa ikiwemo kulizwa 35-12 zilipokutana mara ya mwisho Machi 9, 2019 nchini Canada katika mechi za makundi.

Tangu mwaka 2011, Kenya imezimwa na Ufaransa mara 20 ikiwemo mechi tatu zilizopita na kushinda 19 ikiwemo mara ya mwisho 19-15 Januari mwaka huu nchini New Zealand.