Michezo

Shujaa katika zizi moja na Fiji, Ufaransa na Scotland #DubaiSevens

October 26th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA italimana na Fiji, Ufaransa na Scotland katika mechi za Kundi B za duru ya ufunguzi ya Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 ya Dubai Sevens itakayoandaliwa Novemba 30 na Desemba 1, 2018. Droo ilitangazwa na Shirikisho la Raga Duniani (World Rugby) mnamo Oktoba 25.

Kikosi cha Shujaa kimefanyiwa mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na Paul Murunga kuchukua mikoba ya kocha mkuu kutoka kwa Innocent ‘Namcos’ Simiyu, ambaye aliongoza mabingwa hawa wa zamani wa Afrika kukamilisha msimu uliopita kwa alama za kihistoria 104 katika nafasi ya nane.

Mara ya mwisho Kenya ilikutana na Ufaransa mjini Dubai ilipepetwa 24-14 katika mechi za makundi mwaka 2016. Ilipoteza 33-7 dhidi ya Wafaransa hawa katika nusu-fainali ya Bakuli mwaka 2015.

Mara ya mwisho Kenya ililemea Ufaransa mjini Dubai ni mwaka 2013 ilipoilipua 14-5 katika mechi za makundi. Kenya na Fiji zilikutana mjini Dubai mara ya mwisho mwaka 2012.

Mabingwa wa Dubai mwaka 2013 na 2015 Fiji walilemea Shujaa 14-10 katika mechi za makundi. Wakenya kisha walicharaza Wafaransa 15-12 katika mechi ya kuamua mshindi wa medali ya shaba. Kenya ilikutana na Scotland mara ya mwisho mjini Dubai mwaka 2008. Ilibwaga Scotland 38-0 katika mechi ya Kundi B.

Kundi A linaleta pamoja mabingwa mara sita wa Dubai Sevens Afrika Kusini, ambao pia wanatetea taji, Argentina, washindi wa Dubai Sevens mwaka 2012 Samoa na timu alikwa.

Mabingwa mara sita wa Dubai Sevens New Zealand, ambao hawajatwaa taji la Dubai katika kipindi cha miaka minane, Marekani, Uhispania na Wales wako katika Kundi C.

Wanafainali wa Dubai Sevens mwaka 2014 Australia, mabingwa wa Dubai mara nne Uingereza pamoja na Canada na Japan wanaunda Kundi D.

Raga ya Dunia ya msimu huu inatarajiwa kuwa moto hasa. Timu 15 zinazoshiriki duru zote 10 za ligi zitawania kutwaa ubingwa.

Mataifa manne ya kwanza pia yatafuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 2020. Kwa kawaida timu inayomaliza katika nafasi ya 15 hutemwa kwa hivyo vita vya kukwepa ‘shoka’ pia vitakuwa vikali.

Mataifa yanayoshiriki duru zote ni Afrika Kusini, Fiji, New Zealand, Australia, Uingereza, Marekani, Argentina, Kenya, Canada, Samoa, Uhispania, Scotland, Ufaransa na Wales zilizomaliza msimu 2017-2018 katika usanjari huo.

Urusi ilitemwa na nafasi yake kujazwa na Japan, ambayo ilishinda mchujo wa kupandishwa daraja kushiriki duru zote mjini Hong Kong mwaka 2017. Timu ya 16 huwa inaalikwa na World Rugby.

Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 itaanzia Dubai katika nchi ya Milki za Kiarabu (Novemba 30 na Desemba 1) na kuzuru miji ya Cape Town (Desemba 8-9, Afrika Kusini), Hamilton (Januari 26-27, 2019, New Zealand), Sydney (Februari 2-3, 2019, Australia), Las Vegas (Machi 1-3, 2019, Marekani), Vancouver (Machi 9-10, 2019, Canada), Hong Kong (Aprili 5-7, 2019, Uchina), Singapore (Aprili 13-14, 2019, Singapore), London (Mei 25-26, 2019, Uingereza) na kukamilika Juni 1-2 mjini Paris (Ufaransa).