Michezo

Shujaa kumenyana na Fiji na Ufaransa tena

March 5th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MAKUNDI ya Raga za Dunia ya duru ya Vancouver Sevens yametangazwa, ambapo Kenya itafufua uhasama dhidi ya Fiji na Ufaransa tena.

Shujaa imetiwa katika Kundi C pamoja na Fiji na Ufaransa, ambazo ilikutana nazo katika duru iliyokamilika mjini Las Vegas nchini Marekani, Jumapili.

Ilishangaza Fiji 17-14 na kulimwa 19-14 na Ufaransa mjini Las Vegas. Mbali na Fiji na Ufaransa, Kenya pia itakabiliana na Uhispania katika mechi za makundi za duru hiyo ya sita.

Vijana wa kocha Innocent Simiyu, ambao walimaliza Las Vegas Sevens katika nafasi ya saba kwa alama 10, walimenyana na Uhispania mara ya mwisho msimu 2013-2014. Shujaa ilishinda Uhispania 12-7 katika nusu-fainali ya Ngao ya duru ya Hong Kong Sevens mnamo Machi 30, 2014.

Uhispania ilitemewa mwisho wa msimu huo baada ya kumaliza katika nafasi ya mwisho. Imerejea kwenye ligi hii ya mataifa 15 msimu huu wa 2017-2018. Mara ya mwisho Kenya ilikutana na Uhispania katika ziara ya Amerika Kaskazini ilikuwa Januari 25 ambapo Shujaa iliwika 24-0 katika robo-fainali ya Bakuli.

 

MAKUNDI

A – Marekani, Australia, Canada na Uruguay;

B – Argentina, Uingereza, Wales na Samoa;

C – Fiji, Kenya, Ufaransa na Uhispania;

D – Afrika Kusini, New Zealand, Scotland na Urusi.