Michezo

Shujaa kumenyana na USA, Canada na Ufaransa duru ya Sydney

January 29th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHUJAA ya Kenya imekutanishwa na Marekani ya Mike Friday, Canada na Ufaransa katika mechi za Kundi B za duru ya nne ya Raga ya Dunia itakayofanyika mjini Sydney, Australia mnamo Februari 2-3, 2019.

Vijana wa kocha Paul Murunga wametua nchini Australia kutoka nchini New Zealand walikoshiriki na kumaliza duru ya Hamilton Sevens katika nafasi ya 10 kwa alama saba.

Watafungua kampeni katika siku ya kwanza ya mashindano Februari 2 dhidi ya Canada (1:44am), wavaane na Marekani (7.34am) halafu wafunge siku dhidi ya Ufaransa (11.17am).

Kenya inajivunia kuwa na historia nzuri dhidi ya Marekani na Ufaransa nchini Australia, lakini swali ni je, itafaulu kusonga mbele kutoka kundi hili kwa kuendeleza rekodi yake wakati huu inachechemea?

Inajivunia kuchapa Ufaransa mara tatu ikiwemo mara ya mwisho zilikutana mjini Sydney kwa alama 17-14 mwaka 2018, na kupoteza mara moja, ambayo ilikuwa mara ya kwanza zilikutana nchini Australia mwaka 2007 kwa alama 33-24.

Kenya na Marekani zimelimana mara tatu nchini Australia. Shujaa ilipoteza 17-10 zilipokutana mara ya kwanza mwaka 2011 katika fainali ya Bakuli. Ililemea Marekani 31-5 katika mechi za makundi mwaka 2013 na tena kubwaga Waamerika hao japo pembamba 24-21 katika nusu-fainali ya Sahani mwaka 2016.

Wakenya hawajawahi kushinda Canada nchini Australia katika raga hii ya dunia. Walizabwa 40-7 walipokutana na Waafrika hawa kwa mara ya kwanza nchini Australia mwaka 2014 katika fainali ya Ngao. Taifa hilo kutoka Amerika Kaskazini lililemea Kenya tena 10-5 zilipokutana katika awamu sawa na hii mwaka 2017. Ziara za mwaka 2017 na 2014 zinasalia kuwa mbaya zaidi katika safari za Kenya nchini Australia kwenye Raga ya Dunia.

Kenya ilianza vibaya msimu huu wa 2018-2019 kwa kuambulia alama moja katika duru ya Dubai kabla ya kujiongezea alama tatu mjini Cape Town. Duru hizo zilifanyika Desemba mwaka 2018. Kenya kisha iliimarisha matokeo yake katika duru ya tatu mjini Hamilton nchini New Zealand mnamo Januari 26-27, 2019 pale ilipozoa alama saba ikipoteza 36-7 dhidi ya Uingereza katika fainali ya Challenge Trophy.

Shujaa sasa ina jumla ya alama 11 kutoka duru tatu. Zinasalia duru saba. Iliruka juu nafasi moja hadi nambari 13 baada ya ziara ya New Zealand. Bado ina kibarua kigumu kujinasua kutoka nafasi ya 15 ambayo ni ya kushushwa ngazi.

Makundi ya Sydney Sevens (2019):

A – Fiji, Samoa, Uingereza, Japan

B – Marekani, Canada, Kenya, Ufaransa

C – New Zealand, Scotland, Uhispania, Wales

D – Afrika Kusini, Australia, Argentina, Tonga

Historia ya Kenya dhidi ya Ufaransa, Canada na Marekani katika duru ya Australia 7s:

2018 – Kenya 17-14 Ufaransa (mechi za makundi)

2017 – Kenya 5-10 Canada (fainali ya kutafuta nambari 13)

2016 – Kenya 24-21 Marekani (Nusu-fainali ya Sahani)

2014 – Kenya 7-40 Canada (Fainali ya Ngao)

2013 – Kenya 31-5 Marekani (mechi za makundi)

2011 – Kenya 24-10 Ufaransa (Nusu-fainali ya Bakuli), Kenya 10-17 Marekani (Fainali ya Bakuli)

2008 – Kenya 21-12 Ufaransa (mechi za makundi)

2007 – Kenya 24-33 Ufaransa (mechi za makundi)