Shujaa, Lionesses wala rungu kali fainali ya Madrid Sevens

Shujaa, Lionesses wala rungu kali fainali ya Madrid Sevens

Na GEOFFREY ANENE

TIMU za taifa za raga ya wachezaji saba kila upande za Kenya Shujaa na Lionesses zilipokea vichapo vikali dhidi ya Argentina na Urusi mtawalia katika fainali ya Madrid Sevens, Jumapili.

Shujaa, ambayo ilimaliza duru ya ufunguzi ya Madrid Sevens katika nafasi ya pili mnamo Februari 21, ililazimika kukubali nafasi hiyo tena baada ya kuchabangwa 45-7 na Argentina katika fainali ya wanaume.

Dakika chache awali, Lionesses ilikuwa imekung’utwa 19-0 na Urusi katika fainali ya kinadada.

Lionesses, ambayo ilivuta mkia wikendi iliyopita ilipopoteza michuano yake yote, ilifika fainali ya duru ya pili baada ya kupoteza dhidi ya Urusi 17-5 na Poland 12-10 na kuaibisha wenyeji Uhispania 22-0. Janet Okelo na Christabel Olindo walifunga mguso mmoja kila mmoja dhidi ya Poland ambayo mchezaji wake mmoja alikula kadi ya njano katika kipindi cha kwanza. Mkenya Celestine Masinde alionyeshwa kadi ya njano katika kipindi cha pili.

Katika mechi mbili za mwisho za awamu ya kwanza za Shujaa zilizopigwa Jumapili, vijana wa Simiyu walizamisha Chile 15-5 kupitia miguso ya Vincent Onyala, Tony Omondi na William Ambaka. Walipoteza dhidi ya Argentina 36-19 katika mechi ya mwisho ya awamu hiyo ambayo Jacob Ojee alichangia miguso miwili, mmoja ukiandamana na mkwaju kutoka kwa Daniel Taabu, naye Bush Mwale akafunga mguso mmoja.

Katika fainali, Shujaa iliona cha mtema kuni dhidi ya Argentina ambayo ilioongoza 33-0 kabla ya Onyala kufungia Wakenya mguso mmoja wa kufutia machozi. Taabu alipachika mkwaju wa mguso huo. Baada ya duru hizo mbili zilizofanyika bila mashabiki kutokana na janga la virusi vya corona, Shujaa na Lionesses zinatarajiwa kurejea nyumbani kabla ya kuelekea Dubai kwa duru nyingine mbili mwisho wa mwezi Machi.

Mashindano haya ni ya kusaidia timu kujiandaa kwa michezo ya Olimpiki.

 

You can share this post!

King’ara asambaza viti vya magurudumu Githurai kwa watoto...

Bingwa mara mbili wa Safari Rally Hannu Mikkola afariki