Michezo

Shujaa matumaini tele watawika raga ya Hong Kong 7s

April 4th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA mshikilizi wa kikosi cha Shujaa, Jeff Oluoch ni mwingi wa matumaini kwamba kikosi chao kitatamba katika duru ijayo ya Raga ya Dunia itakayoandaliwa jijini Hong Kong, China wikendi hii.

Timu hiyo ya Kenya ya Raga ya wachezaji saba kila upande imetiwa katika zizi moja na miamba wa dunia Fiji, New Zealand na Australia.

Chini ya kocha Paul Murunga, Shujaa wamekuwa wakisuasua pakubwa katika kampeni za Raga ya Dunia msimu huu, huku matokeo yao duni yakiwaweka katika hatari ya kuteremshwa daraja.

Kwa sasa, kikosi hicho ambacho kimekosa huduma za wachezaji nyota kutokana na mzozo kati yao na Shirikisho la Raga (KRU), kinashikilia nafasi ya 14 jedwalini kwa pointi 18 pekee.

Katika jumla ya duru sita zilizopita za Raga ya Dunia, Shujaa wameshindwa kupiga hatua na kufikia robo-fainali za kuwania Kombe Kuu la Raga (Main Cup).

Nafuu zaidi kwa kikosi cha Shujaa kwa sasa ni kurejea kwa wachezaji wazoefu na wenye tajriba pana katika ulingo wa raga ya kimataifa baada ya KRU kuafikiana nao kuhusu mikataba.

“Ingawa tumetiwa katika kundi gumu zaidi katika raga ya Hong Kong 7’s, tuna wingi wa matumaini ya kutamba na kurejesha Kenya kileleni mwa ramani ya mchezo huo duniani,” akasema Oluoch.

Kenya watafungua kampeni zao dhidi ya Fiji hapo kesho kabla ya kukamilisha michuano yao ya makundi mnamo Jumamosi dhidi ya New Zealand na Australia. Mechi za raundi ya mwondoano zimeratibiwa kupigwa mnamo Jumapili.

Oluoch aliwajibikia kikosi cha Shujaa kwa mara ya mwisho mnamo Disemba wakati Raga ya Dunia ilipoandaliwa Dubai. Nyota huyo amekuwa tegemeo kubwa kambini mwa Homeboyz katika kampeni za kuwania ubingwa wa Kenya Cup msimu huu.

Kwa mujibu wa Eric Ogweno ambaye ni Meneja wa Timu, wachezaji wazoefu wa Shujaa watakuwa sehemu muhimu ya kampeni za kikosi hicho wikendi hii na wikendi ijayo katika duru ya Singapore, Malaysia.

Kikosi cha Shujaa kiliondoka humu nchini kuelekea Hong Kong mnamo Jumanne kupitia Bangkok. mwaka jana, Kenya ilitinga fainali ya Raga ya Dunia japo ilizidiwa maarifa na Fiji iliyosajili ushindi wa 31-12.

Haiba

Shujaa imekuwa bila wachezaji 14 wa haiba kubwa kambini mwao tangu mwanzoni mwa msimu huu wa 2018-19 katika kampeni za raga ya dunia.

Tatizo hili lilikuwa zao la kutofautiana kwa KRU na wanaraga hao kuhusu masuala ya kandarasi zilizoshuhudia mishahara yao ikipunguzwa kwa asilimia kubwa.

Miongoni mwa 14 hao ni Collins Injera, Andrew Amonde, Eden Agero, Samuel Oliech, Billy Odhiambo, William Ambaka, Nelson Oyoo, Dennis Ombachi, Leonard Mugaisi na Dan Sikuta.

Mbali na kuvuta mkia katika duru ya Vancouver Sevens nchini Canada, walipoteza mechi tano mfululizo kwa kupepetwa 47-7 na Australia katika robo-fainali ya Challenge Trophy na 22-14 dhidi ya Japan katika nusu-fainali ya kutafuta mshindi wa nambari 13 hadi 16.

Awali, walizabwa na Fiji (36-12), Samoa (35-12) na Canada (36-21) mechi za makundi. Ni matumaini ya Oluoch kwamba Shujaa itapiga hatua zaidi katika kampeni za duru zijazo za Hong Kong (Aprili 5-7), Singapore (Aprili 13-14), Uingereza (Mei 25-26) na Ufaransa (Juni 1-2).

Kenya imekuwa moja ya timu zinazoshiriki duru zote kwa misimu 16 mfululizo tangu 2002-2003.