Michezo

'Shujaa na Lionesses pamoja na KRU hazitafaidika na hatua ya Rais Kenyatta kupunguza ushuru'

March 27th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga Kenya (KRU) limesema limefurahishwa serikali kuondoa ushuru unaotozwa wananchi wanaokula mshahara wa Sh24,000 kurudi chini kwa asilimia 100 wakati huu mgumu wa virusi vya corona, japo hatua hiyo ‘haitasaidia wachezaji wa timu za taifa za raga za Kenya’.

Katika mahojiano na ‘Taifa Leo‘, Mwenyekiti wa KRU Oduor Gangla alisema, “Kwa kupunguzia watu ushuru, serikali imefanya kitu cha maana. Ni hatua nzuri ya kuondoa ushuru kwa watu wanaopata mshahara usiozidi Sh24, 000. Hata hivyo, wachezaji wetu wanapokea mshahara unaopita kiasi hicho. Kupunguza ushuru wa VAT (kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14) kutasaidia katika bei ya bidhaa kushuka kwa hivyo tunasubiri kwa hamu kubwa kuona bei ya vitu tunatumia kila siku nyumbani ikishuka. Wafanyabiashara kupunguziwa asilimia tano ya ushuru ni kitulizo kikubwa. Inamaanisha kuwa kila mtu anaokoa fedha zaidi, ingawa haibadilishi gharama za KRU kivyovyote.”

Aidha, afisa huyo amekiri kuwa janga la virusi vya corona vimeweka KRU pabaya kwa sababu inaandamwa na majukumu mengi ikiwemo mishahara ya wachezaji wa timu za taifa, ingawa hakuna chochote kispoti watakuwa wakifanya mwezi Aprili, Mei, Juni, Julai na Agosti kwa sababu mashindano yote yamesimamishwa.

Suala la mishahara huwa nyeti, na si mara moja ama mbili, bali mara nyingi timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa, imegoma baada ya mishahara kucheleweshwa ama kupunguzwa.

Alipoulizwa jinsi KRU inapanga kukabiliana na tatizo la kulipa mishahara ya wachezaji kandarasi zao zinavyosema, Gangla alisema, “Tunaishi katika wakati mgumu kwa sababu hakuna fedha mpya zinaingia katika akaunti ya KRU. Kila taasisi imelazimika kufanyia shughuli zake mabadiliko na KRU si tofauti. Matumaini yetu ni kuwa virusi hivi vitadhibitiwa ili maisha yarejelee hali ya kawaida. Tunazungumza na wadau wetu, lakini hali inasalia ya wasiwasi.”

Mwandishi huyu alipotaka kujua ikiwa KRU inawazia kukata mishahara ya wachezaji jinsi klabu nyingi barani Ulaya zimekuwa zikifanya, Gangla alisema, “Kila mtu anafahamu kinachoendelea duniani wakati huu. Kitu muhimu ni kufanya mambo kwa haki.”

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza mabadiliko ya ushuru unaotozwa Wakenya na wakazi wa Kenya hapo Jumatano ili kuwapunguzia changamoto zilizoletwa na virusi vya corona, ambavyo vimeua zaidi ya watu 20,000 duniani na kuambukiza watu zaidi ya 400,000. Vimesimamisha shughuli nyingi ikiwemo michezo na masomo katika taasisi za elimu, miongoni mwa nyingine.