Shujaa na Lionesses wararua wenyeji Uhispania raga ya Madrid Sevens

Shujaa na Lionesses wararua wenyeji Uhispania raga ya Madrid Sevens

Na GEOFFREY ANENE

TIMU za taifa za raga ya wachezaji saba kila upande za Kenya Shujaa na Lionesses zimekamilisha siku ya kwanza ya duru ya pili ya Madrid Sevens kwa kupiga wenyeji Uhispania jijini Madrid, Jumamosi.

Shujaa ya kocha Innocent ‘Namcos’ Simiyu, ambayo ilimaliza duru ya ufunguzi nyuma ya Argentina wikendi ya Februari 20-21, ilitolewa jasho na Uhispania kabla ya kushinda pembamba 19-17.

Dakika chache baadaye, Lionesses, ambayo ilivuta mkia wikendi iliyopita ilipopoteza michuano yake yote, ilionyesha kuimarika zaidi kabla ya kuduwaza Uhispania 22-0.

Mabingwa wa duru ya Raga ya Dunia ya Singapore mwaka 2016 Shujaa walifungua siku kwa kupepeta Ureno 26-12. Walizaba Amerika ya kocha Mike Friday 29-12 katika mchuano wa pili kabla ya kusukumwa vilivyo na Uhispania iliyoongoza kipindi cha kwanza 12-7. Shujaa imeratibiwa kugaragazana na Chile na Argentina hapo Jumapili saa saba na dakika 20 na saa kumi kasoro dakika 18, mtawalia.

Malkia wa Bara Afrika 2018 Lionesses, ambao wako chini ya kocha Felix Oloo, walianza siku kwa kupoteza 17-5 dhidi ya mabingwa wa duru ya kwanza ya Madrid, Urusi kabla ya kubomoa Uhispania. Itakumbukwa kuwa Lionesses waliaibishwa 41-0 walipokutana na Urusi juma moja lililopita.

Baadhi ya wachezaji waliong’ara katika timu za Kenya katika siku ya kwanza ni Billy Odhiambo (Shujaa) na Janet Okelo (Lionesses).

JEDWALI (Februari 27):

Wanaume – Argentina (alama tisa), Kenya Shujaa (tisa), Amerika (saba), Uhispania (tano), Chile (tatu), Ureno (tatu);

Wanawake – Urusi (alama tisa), Amerika (sita), Kenya Lionesses (nne), Uhispania (mbili), Poland (moja).

You can share this post!

BURUDANI: Malisaba azidi kukifua kipaji cha uigizaji

Presha ya kazi ya ukocha ni kama oksijeni kwangu –...