Shujaa na Lionesses watiwa katika makundi ya kifo ya Olimpiki

Shujaa na Lionesses watiwa katika makundi ya kifo ya Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Shujaa na Kenya Lionesses zimetiwa katika makundi moto ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Tokyo, Japan kutoka Julai 23 hadi Agosti 8.

Katika droo iliyotangazwa Juni 28, Shujaa ya kocha Innocent “Namcos” Simiyu itafufua uhasama dhidi ya Afrika Kusini, Amerika ya kocha Mike Friday na washiriki wapya kabisa, Ireland, katika Kundi C.

Lionesses ya kocha Felix Oloo itapepetana na New Zealand, Urusi na Uingereza katika Kundi A.

Shujaa ilifuzu kushiriki Olimpiki kwa mara ya pili mfululizo baada ya kushinda Kombe la Afrika mwaka 2019 nao Lionesses walichukua nafasi ya Afrika Kusini baada ya Afrika Kusini kujiondoa.

Wanaraga wa Kenya wamezamia mazoezi katika kambi ya timu ya taifa ya Kenya ilioko katika kituo cha kimataifa cha michezo cha Kasarani.

Shujaa na Lionesses zilishiriki mashindano ya kujipima nguvu mara mbili mjini Madrid nchini Uhispania mwezi Februari halafu zikaelekea mjini Dubai katika Milki za Kiarabu kwa mashindano mengine mawili mwezi Aprili.

Vijana wa Namcos kisha walishiriki mashindano mawili ya Stellenbosch nchini Afrika Kusini mwezi Mei nao Lionesses wakaelekea Tunisia.

Shujaa na Lionesses, ambazo zilisikitisha katika Olimpiki zilizopita kwa kumaliza nafasi ya 11 kati ya mataifa 12 yaliyoshiriki raga mjini Rio de Janeiro nchini Brazil, zilifaa kuenda Los Angeles mnamo Juni 25-26, lakini safari hiyo ikaondolewa kutokana na sababu ambazo Shirikisho la Raga Kenya (KRU) halikusema.

Kundi la Lonesses ni moto kwa sababu New Zealand ni mabingwa wa Raga za Dunia mara sita. Pia, New Zealand wameshinda Kmbe la Dunia mara mbili na walipoteza dhidi ya Australia katika fainali ya Olimpiki 2016. Urusi pia ni wazoefu kwenye Kombe la Dunia na Raga ya Dunia, ingawa wanashiriki Olimpiki kwa mara ya kwanza kabisa. Isitoshe, Urusi ni mabingwa mara saba wa Bara Ulaya. Uingereza nao wameshiriki Kombe la Dunia na walifika katika nusu-fainali mjini Rio de Janeiro.

Shujaa nayo ina rekodi mbovu dhidi ya Afrika Kusini pia itapimwa vilivyo na kocha wake wa zamani Mike Friday na washiriki wapya Ireland wanaojivunia kuwa na wachezaji wepesi wa kasi. Baadhi ya wachezaji katika kikosi cha Kenya kambini ni Collins Injera, Andrew Amonde, William Ambaka na Vincent Onyala ambaye kwa misimu mitatu sasa amekuwa tegemeo katika ufungaji wa miguso.

You can share this post!

Uhuru awapuuza wanaotilia shaka utendakazi wake

Jamhuri ya Czech yaduwaza Uholanzi na kujikatia tiketi ya...