Michezo

Shujaa sasa yahitaji muujiza kusalia katika Raga ya Dunia

May 28th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wanaamini Kenya itahitaji muujiza kusalia kwenye Raga ya Dunia itakayoingia duru ya mwisho jijini Paris nchini Ufaransa mnamo Juni 1-2 baada ya kusikitisha nchini Uingereza, wikendi.

Shujaa ilimaliza mkiani jijini London kwa alama moja na kuteremka nafasi moja chini hadi nambari 14 kwenye ligi hii ya mataifa 15.

Ilishuhudia pia mwanya wa alama kati yake na Japan inayovuta mkia kwa alama 25, ukikatwa kutoka nne hadi mbili.

Mashabiki wamejawa na hofu zaidi hasa baada ya vijana wa kocha Paul Murunga kujipata wametiwa katika kundi gumu sana la Paris Sevens.

Wafalme hawa wa zamani wa Bara Afrika na Singapore Sevens wamekutanishwa na mabingwa mara tatu wa Raga ya Dunia Afrika Kusini, ambao wameshinda mataji mawili yaliyopita jijini Paris, washindi wa Paris Sevens mwaka 1998 Australia, ambao walifika fainali jijini London siku mbili zilizopita, na Wales walioshinda Kombe la Dunia mwaka 2009.

Shabiki Abel Mwombe Murumba alikuwa na maneno mawili tu kwa Shujaa baada ya matokeo ya London na droo ya Paris kufanywa, “Relegation confirmed (Imethibitishwa tutashushwa ngazi).”

Akimjibu Daudi Were aliyeamini Shujaa inaweza kushinda kundi lake jijini Paris, Ouko Njega alisema, “Hiyo ni ndoto…tunatemwa moja kwa moja kutoka Raga ya Dunia.”

Naye Tom Ngugi alisema, “Tutahitaji muujiza kuponea kuangukiwa na shoka… Bila shaka, tuko katika ‘kona mbaya.”

Shujaa itatua Ufaransa na rekodi ya kutoshinda Australia na Afrika Kusini jijini Paris. Mara ya mwisho ilikutana na Australia jijini Paris ilikuwa mwaka 2016 katika nusu-fainali ya Sahani ilipokung’utwa 26-7.

Kabla ya hapo, ilichapwa na Australia 28-15 katika mechi za makundi za Paris mwaka 2004. Imewahi kukutana na Afrika Kusini mara moja jijini Paris ikichabangwa 35-5 mwaka 2006 katika mechi za makundi. Kenya na Wales hazijawahi kukutana jijini Paris.

Msimu huu ulioanza Novemba 30 mwaka 2018 umeshuhudia Shujaa ikibwaga Wales 33-26 katika mechi ya kutafuta nambari 13 hadi 16 mwezi Desemba nchini Afrika Kusini.

Ilipepetwa 29-10 na Afrika Kusini mwezi Januari nchini New Zealand katika mechi za makundi, ikalimwa 19-14 na Wales katika mechi za kutafuta nambari 9-16 mwezi Februari nchini Australia na kuaibishwa na Australia 47-7 katika mechi za kutafuta nambari 9-16 nchini Canada mwezi Machi.

Pia, ililizwa 28-12 na Australia katika mechi za makundi za Hong Kong mwezi Aprili halafu ikachapa Wales 19-14 katika mechi za makundi za Singapore mwezi Aprili. Kenya imepoteza mechi zake nane zilizopita dhidi ya Australia.

Mara ya mwisho ilichapa Australia ni 19-17 mwaka 2017 nchini New Zealand. Vilevile, Shujaa imezamishwa mara 11 mfululizo na Afrika Kusini, ambayo mara ya mwisho ilisalimu amri ilikuwa 14-12 Desemba mwaka 2015.

Katika droo ya duru ya mwisho msimu huu, Fiji italimana na Ireland, Argentina na Uingereza katika Kundi A, Marekeni, Canada, Samoa na Uhispania ziko Kundi C nayo Kundi D inajumuisha Ufaransa, New Zealand, Scotland na Japan.

Mmoja kutoka orodha ya Wales (alama 30), Kenya (27) na Japan (25) atakayemaliza ligi hii ya duru 10 katika nafasi ya 15 baada ya ziara ya Paris atatemwa. Nafasi yake itajazwa na Ireland ambayo ilishinda mchujo wa kupandishwa daraja mjini Hong Kong mwezi Aprili.

Duru ya London ilishuhudia Fiji, Marekani, New Zealand na Afrika Kusini, ambazo zinashikilia nafasi nne za kwanza kwenye Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019, zikiingia Olimpiki mwaka 2020.