Michezo

Shujaa tayari kuanza mazoezi kwa minajili ya Olimpiki za Tokyo, Japan

October 24th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Innocent ‘Namcos’ Simiyu wa timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, amesema kwamba wachezaji wake wataingia kambini kuanzia Novemba, 2020 kwa minajili ya kujifua kwa Michezo ya Olimpiki ya 2021 jijini Tokyo, Japan.

Maandalizi hayo ya Team Kenya yataongozwa na Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) katika maeneo mbalimbali ya humu nchini. Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu wa NOC-K, mojawapo ya maeneo hayo ni uwanja wa Chuo Kikuu cha Kenyatta ambao uliwahi kukaguliwa na wakufunzi Simiyu (wanaraga wa Shujaa), Paul Bitok (wanavoliboli wa kike wa Malkia Strikers), Benjamin Musa (wanamasumbwi wa Hit Squad) na Camilyn Oyuayo (wanaraga wa Kenya Lionesses).

Kufikia Machi ambapo shughuli za michezo zilisitishwa kwa muda humu nchini kwa sababu ya janga la corona, jumla ya wanamichezo 87 kati ya angalau 100 kutoka humu walikuwa wamejikatia tiketi za kunogesha Michezo ya Olimpiki ya Tokyo iliyoahirishwa kutoka Julai-Agosti 2020 hadi Julai 23-Agosti 8, 2021.

Mbali na raga ya wachezaji saba kila, Kenya itawakilishwa kwenye fani nyinginezo katika Olimpiki za 2021 nchini Japan, zikiwemo mbio za marathon, voliboli (wanawake), ndondi, taekwondo (wanawake) na kupiga mbizo (uogeleaji).

Kwa mujibu wa Simiyu, itamwia vigumu kuita kambini wanaraga wapya ikizingatiwa kwamba hakuna kampeni za humu nchini ambazo zimerejelewa ili kumpa jukwaa mwafaka la kuteua wanaraga wa kutegemea.

“Nitategemea wanaraga waliopo kwa sasa katika orodha ya wachezaji wa Shujaa kabla ya kuwaweka kwenye mizani kwa mujibu wa viwango tunavyovihitaji. Tutaongeza orodha hiyo baadaye kwa kuleta wanaraga wapya kwa kuwa baadhi ya wachezaji tulionao kikosini wana mikataba inayoelekea kutamatika,” akasema Simiyu.

Simiyu, 37, aliteuliwa upya na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) mwanzoni mwa Septemba 2020 kunoa timu ya taifa baada ya Paul Feeney wa New Zealand kugura mwezi Juni. Uteuzi wake ulifanywa baada ya mchakato wa kipindi kirefu uliozingirwa na patashika za kila aina.

Kazi hiyo ilivutia jumla ya wakufunzi 14, kati ya hao watatu wakiwa wa humu nchini; Simiyu, Paul Murunga na Dennis Mwanja, aliyeungwa mkono na idadi kubwa ya wanachama wa Bodi ya KRU.