Shujaa yaendea Uhispania kulipiza kisasi raga ya Vancouver 7s

Na GEOFFREY ANENE

Kenya italenga kulipiza kisasi dhidi ya Uhispania kuweka hai matumaini ya kuingia robo-fainali ya duru ya ufunguzi ya Raga za Dunia za wachezaji sana kila upande jijini Vancouver nchini Canada mnamo Septemba 18.

Timu ya Shujaa imefanyiwa mabadiliko makubwa kikosi kilichopoteza 17-14 dhidi ya Uhispania mara ya mwisho zilikutana Vancouver mwaka 2020.

Mfungaji bora wa miguso ya Kenya, Vincent Onyala na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya kufunga miguso mingi kwenye raga hizo Collins Injera pamoja na aliyekuwa nahodha Andrew Amonde ni baadhi ya wachezaji wazoefu watashabikia timu hiyo kwenye runinga.

Amonde alistaafu baada ya Olimpiki 2020. Injera na Onyala hawakufaulu kuingia kikosi cha mwisho cha kocha Innocent “Namcos” Simiyu kitakachokuwa na nahodha mpya Nelson Oyoo.

Kenya pia italimana na Mexico baadaye leo kabla ya kukamilisha mechi za Kundi A dhidi ya miamba Afrika Kusini mapema kesho ambayo pia ni siku ya mwisho ya Vancouver 7s. Jeffrey Oluoch, Alvin Otieno, Billy Odhiambo na Daniel Taabu ni wachezaji pekee kikosini waliokuwa Vancouver mwezi Machi mwaka 2020.

Kikosi cha Shujaa: Nelson Oyoo (Nakuru, nahodha), Jeffrey Oluoch (Homeboyz, nahodha msaidizi), Alvin Otieno (Homeboyz), Timothy Mmasi (MMUST), Herman Humwa (Kenya Harlequin), Harold Anduvati (Menengai Oilers), Willy Ambaka (Narvskaya Zastava, Urusi), Daniel Taabu (Mwamba), Mark Kwemoi (Menengai Oilers), Levi Amunga (KCB), Billy Odhiambo (Mwamba), Derrick Keyoga (Menengai Oilers), Alvin Marube (Impala Saracens).