Shujaa yafanya mazoezi ya kwanza mbele ya mashabiki Japan

Shujaa yafanya mazoezi ya kwanza mbele ya mashabiki Japan

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya Shujaa iliendelea kufanya matayarisho ya Olimpiki 2020 jijini Kurume nchini Japan bila hofu baada ya matokeo ya vipimo vya afya vya hivi punde kuonyesha wote hawana virusi vya corona mapema Julai 18.

Huku wanasoka wawili kutoka Afrika Kusini pamoja na afisa wao mmoja wakipatikana na virusi hivyo hapo jana na pia visa kugunduliwa kambini mwa timu za Nigeria na Czech, vijana wa kocha Innocent “Namcos” Simiyu walifanya mazoezi yao ya kwanza mbele ya mashabiki kwa mara ya kwanza kabisa.

“Tumekuwa na kipindi cha mazoezi ambacho mashabiki wamekubaliwa kuja uwanjani kututazama. Wamekuja kutushangilia, lakini hatukutangamana nao kwa sababu ni muhimu kuzingatia masharti yaliyoko ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Sisi tumepimwa na kufikia leo asubuhi, hakuna kisa chochote cha Covid-19 ambacho kimethibitishwa kambini hapa,” Simiyu alieleza Taifa Jumapili.

Kenya, ambao ni mabingwa wa Kombe la Afrika la raga ya wachezaji saba kila upande walililonyakua kwa kupiga Uganda 29-0 katika fainali mwaka 2019 wakiingia Olimpiki, wataelekea jijini Tokyo hapo Jumanne asubuhi kwa mashindano.

Katika mechi za makundi, Shujaa watapepetana na Afrika Kusini, ambayo Julai 17 iliruhusiwa kuingia kambi ya mazoezi mjini Kagoshima baada ya watu 17 kati ya 18 katika kikosi chake waliosafiri kupatikana hawakutangamana na mgonjwa wa covid-19 aliyegunduliwa kwenye ndege waliyosafiria.

Timu hizo ziko Kundi C pamoja na Amerika na Ireland. Timu ya raga ya wachezaji saba kila upande ya kinadada maarufu Lionesses pia iko nchini Japan kushiriki Olimpiki.

Ilisafiri katika makundi mawili, huku lile la pili likizuiwa Tokyo baada ya abiria mmoja kwenye ndege waliyosafiria kupatikana na virusi hivyo.

You can share this post!

Arsenal na Rangers nguvu sawa kirafiki

Kikwetu FC yatoka nyuma na kuipiga FC Talents 2-1