Michezo

Shujaa yakaribishwa Cape Town Sevens kwa kipigo

December 8th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHUJAA ya Kenya imeanza kampeni yake ya duru ya pili ya Raga ya Dunia ya Cape Town Sevens kwa mguu mbaya baada ya kupoteza 29-12 dhidi ya Uingereza katika mechi ya Kundi C nchini Afrika Kusini, Jumamosi.

Vijana wa kocha Paul Murunga walipata miguso yao kupitia kwa Cyprian Kuto na Leonard Mugaisi huku nahodha Eden Agero akichangia mkwaju.

Uingereza, ambayo ilimaliza duru ya ufunguzi mjini Dubai katika nafasi ya tatu, ilitangulia kuona lango kupitia Ethan Waddleton dakika ya kwanza huku Tom Mitchell akiongeza mkwaju wa mguso huo na kuongoza 7-0.

Hata hivyo, Kenya ilijibu na dozi sawia kupitia kwa mguso wa Kuto na mkwaju wa Agero dakika ya nne. Uingereza ilienda mapumzikoni kifua mbele 12-7 baada ya mfungaji bora katika Raga ya Dunia Dan Norton kupachika mguso bila mkwaju.

Kenya ilianza kipindi cha pili vyema pale ilipofunga mguso kupitia Mugaisi dakika ya nane, lakini ilikosa majibu kwa kasi ya kutisha ya Norton, ambaye aliongeza miguso miwili kabla ya Phil Burgess kuhitimisha. Mitchell aliongeza mkwaju wa mguso wa mwisho.

Katika mechi ya ufunguzi ya kundi hili, Fiji ilipapura Ufaransa 50-0. Fiji ilinyakua taji la Cape Town Sevens mwaka 1999, 2002 na 2005. Nayo Uingereza ilishinda shindano hili la Afrika Kusini mwaka 2003 na 2016. Kenya na Ufaransa hazijawahi kufika fainali nchini Afrika Kusini.

Kenya itarejea uwanjani saa tisa na dakika 20 kuvaana na miamba Fiji katika mechi yake ya pili kabla ya kukamilisha siku dhidi ya Ufaransa saa kumi na mbili na dakika 41.

Shujaa, ambayo ilivuta mkia jijini Dubai hapo Desemba 1 baada ya kushindwa mechi zake zote, ina alama moja katika kundi lake. Fiji inaongoza kwa alama tatu sawa na Uingereza. Ufaransa iko mkiani kwa alama moja.

Raga ya Dunia inajumuisha duru 10. Msimu huu wa 2018-2019 utatumika kuchagua timu zitakazoshiriki michezo ya Olimpiki mwaka 2020. Timu zitakazomaliza msimu katika nafasi nne za kwanza zitaingia Olimpiki.

Nchi itakayokamilisha duru zote 10 katika nafasi ya 15, itatemwa. Kwa sasa, Kenya inashikilia nafasi hiyo ya kuondolewa katika mashindano haya ya kifahari.