MichezoVideo

Shujaa yakiri utakuwa mlima kuwika London na Paris

May 24th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Oscar Ayodi na Dennis Ombachi wamerejea katika kikosi cha Shujaa kitakachoshiriki duru mbili za mwisho za Raga ya Dunia katika miji ya London (Uingereza) na Paris (Ufaransa) mwezi Juni.

Wawili hawa wamekuwa mkekani kwa karibu miezi mitano wakiuguza majeraha. Ayodi alipata jereha la goti katika duru ya pili mjini Cape Town nchini Afrika Kusini mnamo Desemba mwaka 2017. Amerejeshewa majukumu ya nahodha, ambayo Oscar Ouma alikuwa ametwika katika duru za New Zealand, Australia, Marekani, Canada, Hong Kong na Singapore pamoja na Michezo ya Jumuiya ya Madola. Ouma hayuko katika ziara hii ya Bara Ulaya kutokana na majukumu ya kibinafasi.

Ombachi aliumia kifundo katika duru ya kwanza iliyofanyika mjini Dubai katika nchi ya Milki za Kiarabu mapema Desemba mwaka 2017.

Mabadiliko mengine katika kikosi cha kocha Innocent Simiyu ni kurejea kwa Brian Tanga, ambaye alichezea Kenya mara ya mwisho katika duru ya Hamilton nchini New Zealand naye Erick Ombasa atasafiri kama mchezaji wa 13.

Mabadiliko haya makubwa yamechangiwa na kukosekana kwa Ouma pamoja na Samuel Oliech na Daniel Sikuta ambao walishiriki duru mbili zilizopita Hong Kong na Singapore. Oliech anauguza jeraha naye Sikuta ameruhusiwa kuenda kuomboleza kifo cha ndugu yake.

Shujaa inashikilia nafasi ya sita kwenye ligi hii ya mataifa 15 kwa alama 93. Itamenyana na Marekani, Ufaransa na wenyeji Uingereza katika mechi za Kundi C katika siku ya kwanza ya London Sevens uwanjani Twickenham hapo Juni 2.

Katika mahojiano, Simiyu amekiri kibarua kigumu kinasubiri Shujaa jijini London. Aidha, Simiyu amesema yeye na vijana wake watatafuta kutimiza lengo lao la kushinda duru moja msimu huu wa 2017-2018.

Kikosi cha Shujaa:

Wachezaji

Oscar Ayodi, Collins Injera, William Ambaka, Billy Odhiambo, Jeff Oluoch, Herman Humwa, Nelson Oyoo, Brian Tanga, Augustine Lugonzo, Dennis Ombachi na Erick Ombasa.

Benchi la Kiufundi

Innocent Simiyu (kocha mkuu), Will Webster (kocha msaidizi), Geoffrey Kimani (kocha wa mazoezi ya viungo), Lamech Bogonko (daktari wa timu) na Erick Ogweno (meneja wa timu).

Video Gallery