Na GEOFFREY ANENE
Kenya Shujaa walihakikisha taji la mashindano ya raga ya wachezaji saba kila upande linasalia nyumbani baada ya kulipiza kisasi dhidi ya Ujerumani kwa kuichabanga 12-5 katika fainali ya kusisimua ugani Nyayo jijini Nairobi mnamo Jumapili.
Nyota Alvin ‘Buffa’ Otieno na Johnstone Olindi walifungia Shujaa miguso iliyowezesha Kenya kuhifadhi taji. Jack Hunt alipachika mguso wa Ujerumani ambayo ilikuwa ikirejea Safari Sevens tangu 2014. Ni mara ya kwa Shujaa ilitwaa taji tangu 2016, ingawa timu ya pili ya Kenya, Morans ilishinda 2019 kwa kuzaba Afrika Kusini 19-14 ugani RFUEA.
Hapo Jumapili, fainali ilikuwa ngumu kutoka kipenga cha kwanza kabla ya Otieno kufungua ukurasa wa pointi baada ya kuzidia ujanja ulinzi wa Ujerumani na kutimka hadi katika kisanduku cha miguso. Levy Amunga aliongeza mkwaju kuimarisha uongozi hadi 7-0. Hata hivyo, Ujerumani ilijibu na mguso bila mkwaju sekunde chache baadaye kupitia Jack Hunt, huku Shujaa ikienda mapumzikoni 7-5.
Wajerumani walirejea kipindi cha pili kwa nguvu, ingawa vijana wa kocha Innocent Namcos Simiyu walilinda ngome yao vyema, hata baada ya kubaki wachezaji sita kufuatia Collins Shikoli kulishwa kadi ya njano.
Vijana wa kocha Damian McGrath walizamishwa kabisa na mguso wa Olindi 12-5. Ingawa Amunga alikosa mkwaju wa mguso huo, muda ulikuwa umeisha. Makala ya 2020 hayakufanyika kwa sababu ya mkurupuko wa virusi vya corona.
Kenya Lionesses I ilinyakua taji la kinadada baada ya kupiga wapinzani wote – Titans kutoka Afrika, Kenya Lionesses II, Zimbabwe na Uganda. Lionesses I ilikamilisha kampeni yake kwa kulipua Uganda Lady Cranes 26-0 kupitia kwa miguso ya Janet Okello (miwili), Christabel Lindo na nahodha Philadelphia Olando na mikwaju ya Grace Adhiambo.
Kenya Lionesses II iliridhika na nafasi ya pili nayo Uganda inakamata nambari tatu na kupokezwa tuzo hiyo na mshikilizi wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100, Ferdinand Omurwa Omanyala.
Matokeo ya Oktoba 31:
Robo-fainali
Kenya Morans 21 Samurai 17
Shujaa 19 Uganda 12
KCB 10 Red Wailers 21
Zimbabwe 14 Ujerumani 31
Nusu-fainali
Red Wailers 7 Ujerumani 26
Kenya Morans 17 Shujaa 19
Fainali ya nambari 11:
SA All Stars 7s Academy 19 Nigeria Stallions 12
Fainali ni nambari tisa:
Kenya U20 (Chipu) 21 Uhispania 33
Nusu-fainali za kuorodheshwa 9-12:
Chipu 19 Nigeria Stallions 0, SA All Stars 7s Academy 5 Uhispania 19
Fainali ya nambari saba:
Samurai International 31 KCB 17
Nusu-fainali za kuorodheshwa nambari 5-8:
Uganda 17 Samurai International 14, KCB 0 Zimbabwe 24,
Fainali ya nambari tano:
Uganda 29 Zimbabwe 12
Mechi ya kuamua mshindi wa medali ya shaba:
Red Wailers 5 Morans 12
Mechi ya kuamua bingwa:
Kenya Shujaa 12 Ujerumani 5