Shujaa yapigwa na Great Britain kumaliza raga ya Dubai 7s katika nafasi ya sita

Shujaa yapigwa na Great Britain kumaliza raga ya Dubai 7s katika nafasi ya sita

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Shujaa imekamilisha duru ya pili ya Raga za Dunia za msimu 2021-2022 katika nafasi ya sita jijini Dubai nchini Milki za Kiarabu, Jumamosi.

Hii ni baada ya kupoteza dhidi ya Great Britain kwa alama 10-5 katika fainali ya kuamua nambari tano na sita.

Vijana wa kocha Innocent “Namcos” Simiyu walitangulia kuona lango kupitia mguso wa Jeffrey Oluoch dakika ya nne baada ya kupokea pasi murwa kutoka kwa Johnstone Olindi na kutimka hadi kisanduku cha miguso.

Great Britain ilijibu na mguso kupitia kwa Robbie Fergusson kabla ya mapumziko kabla ya kuzamisha Kenya katika kipindi cha pili.

Kichapo hicho ni cha tatu mfululizo cha Kenya mikononi mwa Great Britain ambayo ilitamba 31-7 zilipokutana kwenye Olimpiki 2016 jijini Rio de Janeiro, Brazil na kutawala 33-5 katika duru ya kwanza ya Dubai Sevens msimu huu mwezi uliopita.

Baada ya Dubai, mashindano haya ya raga ya wachezaji saba kila upande yataelekea nchini Uhispania kwa duru mbili zijazo. Duru hizo zitafanyika mjini Malaga mnamo Januari 21-23 na mjini Seville mnamo Januari 28-30.

You can share this post!

Kabras, Strathmore na Menengai Oilers wang’aria wenyeji...

Nyundo ya West Ham United yazamisha Chelsea ligini

T L