Michezo

Shujaa yapata mkurugenzi mpya Paul Feeney, kocha Paul Murunga gizani

September 20th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga la Kenya limeajiri raia wa New Zealand, Paul Feeney kusimamia timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume almaarufu Shujaa.

Feeny, 56, pia atasaidia timu ya taifa ya wachezaji 15 kila upande ya wanaume ya watu wazima (Simbas) na chipukizi (Chipu) pamoja na timu ya wanawake (Lionesses) katika kuimarisha ujuzi wa timu hizo na idara ya ulinzi.

Ikitangaza uteuzi wa Feeney, ambaye alianza kazi ya ukocha mwaka 1995, KRU imesema pia kandarasi yake ni ya miaka miaka minne itakayokatika baada ya Kombe la Dunia mwaka 2022.

“Feeney ni kocha aliyehitimu na kiwango tatu cha Shirikisho la Raga Duniani mwenye zaidi ya miaka 25 ya ujuzi katika kazi ya kunoa raga ya wachezaji 15 kila upande pamoja na raga ya wachezaji saba kila upande hadi viwango vya juu.

“Alishinda Kombe la Dunia la raga ya wachezaji saba kila upande mwaka 2005 akiongoza Fiji na pia alifanya kazi na timu ya taifa ya New Zealand hasa ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka 2014 na 2015.

“Mbali na timu za taifa, Feeney amefundisha timu ya Auckland ITM kwa misimu minne na kutwaa mataji mawili ya kitaifa nao katika raga ya wachezaji saba kila upande. Kazi yake ya mwisho kabla ajiunge nasi ilikuwa naibu wa kocha wa timu ya Stormers kwa misimu mitatu akishughulikia kuimarisha ujuzi wa timu na idara ya ushambuliaji,” KRU imesema Ijumaa.

Kazi ya kwanza ya Feeney, KRU imesema, ni kusaidia timu ya Shujaa kufuzu kushiriki Olimpiki mwaka 2020.

Kenya itapigania tiketi ya kushiriki Olimpiki ya wanaume dhidi ya Zimbabwe, Uganda, Madagascar, Zambia, Tunisia, Senegal, Morocco, Namibia, Ghana, Botswana, Mauritius, Ivory Coast na Nigeria katika Kombe la Afrika mnamo Novemba 8-9, 2019 nchini Afrika Kusini.

Lionesses ilishinda Kombe la Afrika mwaka 2018. Itawania taji hili tena mwaka 2019 ikitafuta kuwa katika Olimpiki. Itamenyana na Uganda, Zimbabwe, Madagascar, Senegal, Botswana, Zambia, Morocco, Mauritius, South Africa, Ghana na wenyeji Tunisia mnamo Oktoba 12-13, 2019.

Tangazo la kuajiri Feeney bila ya kuzungumzia kocha wa Shujaa, Paul Murunga, linawacha Wakenya gizani wasijue amepigwa kalamu ama la. Hata hivyo, ripoti za Murunga kuangukiwa na shoka zimekuwa zikizunguka tangu timu hiyo iponee chupuchupu kutemwa kutoka Raga ya Dunia msimu 2018-2019 hapo mwezi Juni.