Michezo

Shujaa yapiga Afrika Kusini, yasonga hatua 1

January 27th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa iliingia mduara wa 10-bora kwenye Raga ya Dunia baada ya kujizolea alama 10 muhimu Jumapili kutokana na duru ya Hamilton nchini New Zealand.

Shujaa ilitua Hamilton ikishikilia nafasi ya 11 kwenye ligi hii ya mataifa 15 na duru 10. Sasa ina jumla ya alama 25 baada ya kupoteza dhidi ya Argentina 19-17 katika mechi ya kutafuta nambari saba na nane.

Vijana wa Paul Feeney walianza kampeni yao vibaya walipotupa uongozi wa alama 19-5 na kulemewa 24-19 na Uingereza katika mechi ya kwanza ya Kundi B usiku wa kuamkia Jumamosi.

Mambo yalionekan kuwa mabaya zaidi Shujaa ilipokabwa 12-12 dhidi ya timu ya kualikwa Japan katika mechi ya pili mapema Jumamosi.

Hata hivyo, iliamka katika mechi yake ya mwisho ya kundi hilo dhidi ya Afrika Kusini usiku wa kuamkia Jumapili ilipomaliza nuksi za kuchapwa mara 14 mfululizo kwa kunyamazisha mabingwa hao wa duru ya Dubai kwa alama 36-14.

Kenya, ambayo mara ya mwisho kubanabana Afrika Kusini ilikuwa Desemba 12 mwaka 2015 iliponyamazisha miamba hao 14-12 mjini Cape Town, ililipiza kisasi kwa kufunga miguso sita dhidi ya miwili.

William Ambaka na Geoffrey Okwach walifunga miguso miwili ya kwanza kabla ya Collins Injera kuongeza wa tatu, huku Kenya ikiongoza 19-0 baada ya Johnstione Olindi kuchangia mikwaju miwili.

Afrika Kusini ilipata mguso kutoka kwa Muller du Plessis na mkwaju wake kupitia kwa Branco du Preez na kuenda mapumzikoni alama 19-7 nyuma.

Jeffery Oluoch aliimarisha uongozi wa Kenya hadi 22-7 mapema katika kipindi cha pili kupitia mguso bila mkwaju. Zain Davids alipunguza mwanya huo kwa kufunga mguso ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Selvyn Davids. Hata hivyo, Alvin Otieno na Vincent Onyala walihakikishia Kenya ushindi huo mnono walipoongeza mguso mmoja kila mmoja, huku Daniel Taabu akichangia mkwaju.

Nelson Oyoo, Injera na Ambaka walifungia Kenya miguso mitatu ikipoteza dhidi ya Argentina.

Timu hiyo kutoka Amerika ya Kusini ilipata idadi sawa ya mikwaju, lakini ikafunga mikwaju miwili ikilinganishwa na Kenya iliyopata mkwaju kupitia Olindi.

Wenyeji New Zealand walizaba Ufaransa 27-5 katika fainali nao Australia wakalima Uingereza 33-21 katika mechi ya kuamua mshindi wa medali ya shaba. Duru ijayo itakuwa mjini Sydney nchini Australia mnamo Februari 1-2.

Jedwali la Hamilton Sevens: New Zealand (alama 22), Ufaransa (19), Australia (17), Uingereza (15), Canada (13), Marekani (12), Argentina (11), Kenya (10), Fiji (8), Afrika Kusini (7), Scotland (6), Ireland (5), Uhispania (4), Japan (3), Samoa (2), Wales (1). Msimamo wa Raga za Dunia baada ya Hamilton Sevens: New Zealand (alama 63), Afrika Kusini (48), Ufaransa (48), Uingereza (39), Australia (35), Argentina (35), Fiji (31), Marekani (30), Canada (26), Kenya (25), Ireland (22), Samoa (21), Scotland (19), Uhispania (13), Japan (6), Wales (4).