Shujaa yaridhika nambari mbili Madrid 7s Lionesses ikivuta mkia

Shujaa yaridhika nambari mbili Madrid 7s Lionesses ikivuta mkia

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilikamilisha mashindano ya kwanza ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Madrid Sevens ya wanaume katika nafasi ya pili na nambari sita (mwisho) katika kitengo cha wanawake nchini Uhispania, Jumapili.

Shujaa ilipoteza 21-14 mikononi mwa Argentina katika fainali ya wanaume ya duru hiyo iliyofanyika Februari 20-21.

Vijana wa kocha Innocent ‘Namcos’ Simiyu walianza fainali vibaya wakati nahodha Nelson Oyoo alilishwa kadi ya njano kwa kucheza visivyo dakika ya kwanza na kukaa nje dakika mbili.

Argentina ilikuwa karibu na maeneo hatari ya Kenya wakati wa adhabu hiyo na ilitumia fursa hiyo kuanzisha mpira kwa haraka na kupachika mguso katikati ya milingoti ulioandamana na mkwaju wake.

Oyoo alijerea uwanjani Shujaa ikifanya shambulizi, William Ambaka alipasia mpira Tony Omondi ambaye alimegea pasi Oyoo na kutimka hadi ndani ya kisanduku akifunga mguso uliofanya alama kuwa 7-7 baada ya Omondi kuongeza mkwaju.

Argentina ilijibu sekunde chache baadaye baada ya kuona mwanya katika ulinzi wa Kenya na kuutumia kwa haraka kupata mguso wa kujirejesha mbele 12-7. Mkwaju ulikuwa sawa kwa hivyo Argentina iliongoza 14-7.

Shujaa ilianzisha tena mpira vyema na kuumiliki. Johnstone Olindi alitimka kuelekea maeneo ya goli ya Argentina, lakini akakabiliwa na kupoteza fursa hiyo alipogonga mpira akijaribu kusuka pasi huku kipindi cha kwanza kikikatika bila alama zaidi.

Shujaa ilisawazisha 14-14 mapema katika kipindi cha pili kupitia mguso wa Alvin “Buffa” Otieno aliyepokea pasi kutoka kwa Omondi ambaye aliongeza mkwaju wa mguso huo.

Argentina iligonga msumari wa mwisho dakika za lala-salama ilipofunga mguso na mkwaju wake.

Katika mechi za kundi hilo, Shujaa ilipepeta Ureno 36-5, Uhispania 19-5, Amerika ya Mike Friday 38-7 na kupoteza 21-7 dhidi ya Argentina.

Lionesses ilichabangwa 12-10 na wenyeji Uhispania katika mechi ya kuamua nani kati ya wawili hao anavuta mkia.

Vipusa wa kocha Felix Oloo walitangulia kuona lango kupitia mguso wa Stella Wafula aliyechanganya walinzi na kufunga mguso kwenye kona. Nahodha Philadelphia Olando alikosa mkwaju.

Uhispania ilisawazisha kupitia mguso bila mkwaju kutoka kwa Ingrid Algar. Pasi murwa kutoka kwa Christabel Lindo ilishuhudia Janet Okello akitimka na kufunga mguso wa pili, huku mkwaju ukienda fyongo.

Uhispania ilikamilisha kipindi hicho cha kwanza kifua mbele 12-10 baada ya kuiba pasi mbovu ya Kenya na kufunga mguso na mkwaju. Hakuna aliyeona lango katika kipindi cha pili.

Kichapo hicho kilifanya Lionesses kukamilisha duru hiyo ya kwanza bila ushindi. Ilikuwa imekung’utwa na Urusi 41-0, Ufaransa 63-5, Amerika 29-5, Uhispania 10-7 na Poland 15-7 katika mechi za kundi hilo.

Timu tano zilishiriki kitengo cha wanaume baada ya Ufaransa kujiondoa. Sita ziliwania ubingwa wa kinadada ikiwemo Ufaransa. Urusi ilishinda taji la kinadada. Duru hiyo ilichezeshwa kwa kutumia mfumo wa mzunguko. Duruy a pili itaandaliwa Februari 27-28 mjini Madrid. Mashindano haya, ambayo yatajumuisha duru mbili baadaye mwezi ujao nchini Milki za Kiarabu na mbili nchini Ufaransa mwezi Mei, ni za kuandaa timu kwa michezo ya Olimpiki ama mechi za kufuzu kushiriki Olimpiki. Shujaa na Lionesses zilifuzu kushiriki Olimpiki jijini Tokyo mwaka 2019.

You can share this post!

Watatu waangamia baada ya matatu kupoteza mwelekeo na...

Tottenham wana matatizo mengi ambayo siwezi kutatua –...