Shujaa yasuasua Safari Sevens ikipamba moto

Shujaa yasuasua Safari Sevens ikipamba moto

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Shujaa ilikamilisha siku ya kwanza ya mashindano ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Safari Sevens kwa matokeo mseto, huku Ujerumani, Samurai na Uganda waking’aria kila mpinzani waliyekutana naye ugani Nyayo hapo jana.

Shujaa ilianza mechi za Kundi A kwa kupepeta Stallions ya Nigeria 60-0 kupitia miguso ya Brunson Madigu, Timothy Mmasi, Alvin Otieno, Alvin Marube, Edmund Anya, Herman Humwa, Johnstone Olindi na Archadius Khwesa naye Levy Amunga akapchika mikwaju mitatu.

Vijana wa kocha Innocent ‘Namcos’ Simiyu walitupa uongozi wa 12-0 wakiduwazwa 14-12 na Ujerumani katika mechi ya pili ya pili. Otieno na Anya walifunga mguso mmoja kila mmoja naye Olindi akaongeza mkwaju kabla ya mapumziko.

Ujerumani ilirejea kipindi cha pili ikiwa mnyama tofauti na kuvuna ushindi kupitia miguso ya Leon Hees na Max Roddick na mikwaju yake kutoka kwa Robin Pluempe na Roddick. Ilinufaika pia na Olindi kukalishwa nje dakika mbili baada ya kuonyeshwa kadi ya njano.

Shujaa ilijikatia tiketi ya robo-fainali kwa kuzaba Zimbabwe 26-5 kupitia miguso ya Olindi (miwili) na nahodha Humwa na Marube na mikwaju ya Amunga. Zimbabwe ilijiliwaza na mguso kutoka kwa Christopher Vuyani.

Washindi wa Kundi C Uganda na nambari mbili na mabingwa watetezi Morans walijikatia tiketi za robo-fainali. Morans ilianza kampeni yake kwa kuaibishwa 24-0 mikononi mwa Uganda inayonolewa na Mkenya Tolbert Onyango.

Ilitoka 12-12 dhidi ya mabingwa wa kitaifa KCB kabla ya kufuzu kwa kuzima Uhispania 31-21. Mabingwa wa zamani Samurai wanayochezea nyota Collins Injera na Andrew Amonde walimaliza juu ya Kundi B baada ya kulipua Kenya Under-20 (Chipu) 38-7, Red Wailers 38-0 na SA All Star Academy kutoka Afrika Kusini 31-12.

You can share this post!

Nassir amrushia Shahbal fataki kali

K’Ogalo juu ya meza Tusker wakionja ushindi wa kwanza

T L