Habari Mseto

Shule hazitafungwa licha ya corona kusambaa zaidi – Serikali

October 29th, 2020 1 min read

CHARLES WASONGA NA VALENTINE OBARA

SERIKALI imesisitiza kuwa shule hazitafungwa licha ya virusi vya corona kuzidi kuongezeka katika siku za hivi karibuni, ambapo walimu 33 wameambukizwa virusi hivyo.

Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang’ jana aliwaambia wabunge kwamba wafanyakazi wanne wa shule pia wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo.

Dkt Kipsang’ alieleza kuwa jumla ya shule 35 kote nchini zimenakili visa vya ugonjwa huo. Hata hivyo, alitupilia mbali uwezekano wa shule kufungwa kutokana na hali hiyo.

“Licha ya visa ya maambukizi kuripotiwa miongoni mwa walimu na wanafunzi, masomo yataendelea kwani hatuna mipango ya kufunga shule tena. Visa hivyo vitashughulikiwa tukijadiliana na Wizara ya Afya kuhusu hatua za kufunguliwa kwa madarasa mengine,” Dkt Kipsang’ akaeleza.

Mnamo Jumapili Waziri wa Elimu George Magoha pia alisisitiza kuwa shule hazitafungwa licha ya ripoti kuhusu maambukizi ya Covid-19.

Baadhi ya washikadau wamekuwa wakihimiza shule kufungwa.Wakati huo huo, Prof Magoha jana alisema agizo la serikali kwamba shule zifunguliwe kwa wanafunzi wa Darasa la Nne, Nane, na Kidato na Nne linafaa kutekelezwa na shule zote.

Shule zinazotumia mtaala wa kimataifa zilikuwa zimepanga kuruhusu wanafunzi wote kurejea shuleni kuanzia Jumatatu wiki hii, lakini mpango huo ukabatilishwa wakati ilipobainika kwamba maambukizi ya virusi vya corona yanapanda kwa kasi.

“Kama kuna mtu yeyote anayeruhusu watoto zaidi ya wale tulioruhusu shuleni, tutawaadhibu. Hili ni onyo kwa yeyote anayedhani ana nguvu kuliko serikali. Kesho nitahitaji kukabidhiwa ripoti kamili kuhusu suala hilo na tusilaumiwe kwa hatua yoyote tutakayochukua,” akasema.

Akizungumza katika ziara Kaunti ya Nyeri, waziri huyo alisisitiza kuwa maagizo yanayotolewa kuhusu elimu yanahusu shule zote, iwe ni za umma au za kibinafsi.

“Watoto wote ni sawa, bila kujali shule wanakosoma,” akasema.