Habari Mseto

Shule hii inatulazimu tulipe Sh44m ilizokopa, wazazi walia

June 30th, 2019 2 min read

Na CHARLES WANYORO

WAZAZI wa Shule ya Upili ya Wasichana ya St Mary’s Igoji wamemwandikia waziri wa Elimu George Magoha kuingilia kati, baada ya wanafunzi 600 kutumwa nyumbani kuleta pesa za kugharamia deni la Sh44 milioni ambalo shule hiyo ilikopa benki miaka saba iliyopita.

Wazazi hao wamesema kuwa pesa hizo zilikopwa kugharimia ujenzi wa bweni, miaka kabla wanafunzi 1200 walioko shuleni humo kujiunga nayo.

Shule inasema kila mzazi anafaa kulipa Sh22,000 kila mwaka kando na karo ya kawaida, hadi wakati mkopo huo utakamilishwa.

Wanafunzi wa vidato vya kwanza, pili na tatu walitumwa nyumbani Jumamosi, nao wa kidato cha nne wakatumwa jana asubuhi, wakihitajika kurejea shuleni watakapokamilisha kulipa pesa hizo.

Mzazi aliyezungumza na Taifa Leo bila kutaka kutambuliwa alisema wazazi wengi hawataki kulipa pesa hizo, kwa kuwa zilikopwa miaka mingi kabla ya wana wao kujiunga na shule hiyo ya kitaifa.

Wengine ambao tayari wameanza kulipa walisema mbinu ambayo inatumiwa inawaumiza kwa kuwa wanalipa nyingi mno na kuwachosha kifedha. Wazazi hulipia wanao Sh50,000 kama karo kwa mwaka, pamoja na Sh2,000 za ushauri.

“Shule haina kitu, si kwa kukosa karo ila kutokana na madeni ambayo hayajaandikwa. Tuliibua malalamishi wakati wa mkutano wa mwaka lakini wazazi wanaoegemea upande wa usimamizi wa shule wakatushinda nguvu,” akasema mmoja wa wazazi.

“Mwalimu Mkuu alisema kuwa alipata deni hilo na kuwa njia ya pekee ya kuisimamia vyema ni baada ya deni lenyewe kulipwa,” akasema.

Mzazi mwingine naye alitaka akaunti ya shule ikaguliwe, akisema huenda kiwango ambacho shule inasema ilikopa si halisi, na inaweza kuwa inaongeza wazazi wagharamike bure.

Mwalimu Mkuu Petronilla Mulwa hakuzungumza na Taifa Leo, lakini Mkurugenzi wa Elimu eneo la Imenti Kusini Mercy Itunga alisema shule hiyo imekuwa ikikumbwa na matatizo kutimiza majukumu yake ya kimsingi, kutokana na hali ya wazazi kutolipa karo.

“Shule hiyo ina changamoto nyingi ambazo hata waziri anazifahamu na hakuna jinsi watoto watasalia shuleni bila kulipa karo. Watakula nini? Wanafunzi walitumwa nyumbani kuwakumbusha wazazi kuhusu majukumu yao,” akasema Bi Itunga.