Habari

Shule kufunguliwa Septemba

June 6th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Shule na taasisi zote za elimu nchini zitarejelea shughuli za masomo muhula wa tatu.

Rais Uhuru Kenyatta Jumamosi amesema uamuzi huo umeafikiwa baada ya kuhusisha wadau mbalimbali katika sekta ya elimu na wizara ya afya.

Kwenye hotuba yake kwa taifa na iliyosubiriwa kwa hamu na ghamu na Wakenya wakitarajia masharti yaliyowekwa kudhibiti maenezi ya ugonjwa wa Covid – 19 yatalegezwa, kiongozi wa nchi ametangaza kuwa shule na taasisi zote za elimu zitafunguliwa Septemba 1, 2020.

“Kufuatia mashauriano kati ya wadau husika sekta ya elimu na wizara ya afya, tumekubaliana masomo yatarejelewa muhula watatu. Zitafunguliwa kuanzia Septemba 1,” Rais Kenyatta akadokeza, katika hotuba yake iliyopeperushwa moja kwa moja kutoka Ikulu, Nairobi, kupitia runinga.

Rais alisema, baada ya kushirikisha wataalamu na watafiti, imeonekana kufungua shule wakati huu maambukizi yanaendelea kuongezeka “ni kama kufungulia virusi nafasi ya kusambaa zaidi”.

Shule na taasisi zote za elimu nchini zilifungwa Machi 2020, Kenya ilipotangaza kuwa mwenyeji wa virusi hatari vya corona, ambavyo sasa vimegeuka kuwa kero la ulimwengu.

Kufuatia mtihani wa kitaifa wa darasa la nane, KCPE na kidato cha nne, KCSE, unaofanywa mwishoni mwa kila mwaka, Rais Kenyatta amesema kwamba wizara ya elimu itatoa ratiba ya mitihani ya mwaka huu katikati ya mwezi Agosti.

Siku kadhaa zilizopita, katibu mkuu wa muungano wa kutetea walimu nchini, KNUT, Wilson Sossion alisema pendekezo la kufungua shule wakati huu maambukizi ya Covid – 19 yanaendelea kuongezeka, ni kuhatarisha maisha ya wanafunzi.

Akieleza kutoridhishwa na kauli ya waliopendekeza shughuli za masomo zirejelewe muhula wa pili, Bw Sossion ambaye pia ni mbunge maalum alisema “elimu si suala muhimu kuliko maisha ya watoto” na kwamba inaweza kusubiri janga la corona lidhibitiwe.