Habari za Kitaifa

Shule kupandisha karo kufuatia serikali kuungama haitafaulu kulipa kiwango kizima

Na WINNIE ATIENO July 1st, 2024 1 min read

WALIMU wakuu watalazimishwa kuongeza karo kuanzia muhula ujao baada ya serikali kuungama inakabiliwa na changamoto za kutoa fedha za kufadhili shughuli za masomo.

Hili ni pigo kwa wazazi ambao watoto wao wanarejea shuleni kuanzia leo baada ya likizo fupi ya wiki moja.

Walimu wakuu watalazimika kusaka njia mbadala za kupata fedha za kukimu mahitaji ya wanafunzi kwani serikali imesema haitakuwa ikituma Sh22, 244 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi wa shule ya upili ya umma bali itatuma Sh17,000 pekee.

“Walimu wakuu watalazimika kukubali Sh17,000 ambazo tumekuwa tukitoa. Serikali haitamudu kutuma Sh22,244 kwa kila mwanafunzi kila mwaka kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi katika shule za upili za umma,” akasema Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu

Akiongea na Taifa Leo, waziri huyo alitoa hakikisho kuwa serikali itahakikisha kuwa fedha za ufadhili wa masomo zinatolewa kwa wakati.

Wiki hii, walimu wakuu walikuwa wamependekeza karo iongezwe kutoka Sh53,000 hadi 69,000 katika shule za upili za kitaifa.

Walisema hii ni kutokana na tatizo la mfumko wa bei za bidhaa unaathiri shule nyingi.

Walimu wakuu walitoa pendekezo hilo mjini Mombasa katika Kongamano lao lililofanyika katika Ukumbi wa Zayed ambako walijadili maswala mbalimbali yanayoathiri sekta ya elimu ikiwemo mtindo wa serikali kuchelewa kutuma fedha za mgao wa kufadhili masomo.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili Nchini (KESSHA) alisema karo ya Sh53,000 inayotozwa katika shule za upili za kitaifa ni finyu mno.

“Tuliwasilisha pendekezo kwa Wizara ya Elimu kwamba karo hii iongezwe hadi Sh69,000 kwa mwaka. Sababu ni kwamba bei za bidhaa zimepanda zaidi,” akasema Bw Kuria ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Murang’a.