Makala

Shule kushiriki shindano la Roboti nchini Uturuki baada ya kuunda moja inayojenga nyumba

Na FRIDAH OKACHI August 15th, 2024 2 min read

SHULE ya Upili ya wasichana ya Mbaikini iliyo na wanafunzi 68 itawakilisha Kenya kwenye shindano la Roboti Duniani, Novemba 28 – 30, 2024 huko Izmir, nchini Uturuki baada ya wanafunzi watatu kutangazwa washindi wa uvumbuzi wa Roboti, iliyo na uwezo wa kujenga nyumba.

Wanafunzi hao wa Kidato cha Kwanza watawakilisha kitengo cha watu wakubwa (Senoir Category), baada ya kushiriki shindano hilo lililoandaliwa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, Nairobi, Agosti 4, 2024.

Wanafunzi hao walikuwa miongoni mwa washindani 25 ambao husoma somo la lugha ya komputa.

Mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza Winnie Wangare, aliambia Taifa Dijitali kwamba ubunifu huo utabadilisha dhana ya wakazi ambao hutaja shule hiyo kuwa na kiwango cha chini cha masomo.

“Watu wengi husema tunasomea shule ya chini sana. Wanafunzi wa shule hii hutajwa kutoka kwenye familia zilizo na umaskini bila kujali  talanta zetu. Wengi huwa na fikra na mazoea ya kusema hatuwezi kuenda mbali au kupata ushindi wowote,” alisema Wangare.

Wanafunzi hao walivumbua roboti ya ujenzi ambayo inatumia lugha ya mashine (code) na ubongo. Roboti hiyo ikiwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi mingi na haraka ikilinganishwa na binadamu.

Bango la shule hiyo iliyo na wanafunzi 68 pekee japo wenye talanta kubwa. Picha|Fridah Okachi

“Tulipewa dakika ishirini kutengeneza nambari (Code) ambazo ziliwezesha roboti hiyo kuwa na uwezo wa kutumia akili na lugha ya kompyuta. Japo, kwa wakati mwingine roboti hiyo ilichelewa kufanya jinsi tuliipangia,” alitabasamu Wangare.

Baada ya kutangazwa kuwa washindi, walielekezwa kwenda kuboresha zaidi uvumbuzi huo ambao uliwapa nafasi ya kuingia kwenye mashindano ya dunia ya roboti.

Hata hivyo, wanakumbwa na changamoto za kugharamia safari yao ya kwenda Uturuki, wazazi wa wanafunzi hao wakiomba mashirika na taasisi za elimu kuwasaidia.

Mamake Anjela Kalondu, mwanafunzi wa kundi la uvumbuzi wa roboti hiyo alisema anatazamia kuona mwanawe akipata viza ili mwanawe kufanikisha ndoto yake.

Mkurugenzi wa elimu katika Shirika la Kenya Connect Bw Patrick Mugoti, aliyefadhili wanafunzi hao, alisema wanapata ugumu wa kugharamia usafiri huo.

“Naomba niweze kupata watu ambao watasaidia watoto hao kufanikisha ushindi huu. Kuna mambo mengi yanayohitajika na hatuyawezi yote,” alisema Bw Mugoti.

Shule ya Mbaikini inapatikana katika eneo bunge la Mwala, uchache wa wanafunzi kujiunga na shule hiyo umetokana na baadhi ya wazazi au wakazi kudai kuwa wanaojiunga ni maskini.

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2021, mwaka huu ikitarajiwa kuwa na watahiniwa watakaokalia mtihani wa Kidato cha Nne kwa mara ya kwanza.