Shule miamba zatupwa nje ya 100 bora

Shule miamba zatupwa nje ya 100 bora

Na WAANDISHI WETU

SHULE za upili zilizokuwa zikiwika kimatokeo katika eneo la Pwani haziko kwenye orodha ya 100 bora kitaifa mwaka huu.

Shule za Upili za Allidina Visram, Aga Khan na Mama Ngina zilizoko Kaunti ya Mombasa, kwa miaka mingi zilikuwa zikiwakilisha Pwani kimatokeo katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE).

Lakini mwaka huu, Pwani nzima imetoa shule mbili pekee za upili ambazo ni za kibinafsi kwenye orodha ya 100 bora kitaifa.

Shule hizo ni Light Academy ambayo imeibuka katika nafasi ya 68 na Sheikh Khalifa Bin Zayed Al-Nahyan katika nafasi ya 91.

Mwaka huu, shule nyingi ndogo zilifanya vyema katika mtihani huo katika kaunti mbalimbali. Katika Kaunti ya Makueni, Shule ya Kyang’ondu Mixed ilishangaza miamba na kuibuka ya kwanza eneo hilo.

Shule hiyo ya daraja la Kaunti Ndogo ilifanikiwa kutoa watahiniwa 65 watakaojiunga na vyuo vikuu, kati ya 70 waliofanya KCSE. Watahiniwa watatu walipata alama A.

Mkuu wa shule hiyo, Tabitha Nzuva alisema kulikuwa na ushirikiano mzuri kati ya walimu huku wanafunzi wakiwa na nidhamu ya hali ya juu.

Shule ya Upili ya Wavulana ya Makueni ilitoa wanafunzi 25 waliopata alama ya A-.

Katika Kaunti ya Murang’a, Shule ya Upili ya Karega Day iliongoza shule nyingine za daraja la Kaunti Ndogo, huku ikishinda baadhi ya shule za Kaunti.

Watahiniwa 86 kati ya 168 waliofanya KCSE shuleni humo walipata alama ya C+ kwenda juu zitakazowawezesha kujiunga na vyuo vikuu.

Shule nyingine iliyoshangaza wengi katika kaunti hiyo ni Edinburg International iliyo mjini Muranga. Ilikuwa mara ya kwanza shule hiyo kuwa na watahiniwa wa KCSE ikaibuka miongoni mwa shule bora zaidi katika kaunti.

Katika Kaunti ya Meru, Shule ya Upili ya Burieruri iliinuka mwaka huu baada ya kupata matokeo mabaya miaka iliyopita.

Shule hiyo ilipata wanafunzi sita wenye alama ya A-, na 11 ambao walipata B+. Jumla ya wanafunzi 70 walipata alama juu ya C+.

Ripoti ya Valentine Obara, Pius Maundu, Ndungu Gachane na Charles Wanyoro

You can share this post!

Watahiniwa walemavu waongezeka, wang’aa

Waliowika KCSE wafichua siri za ufanisi

adminleo