Habari Mseto

Mahakama yaagiza SABIS® International ipunguze karo kwa asilimia 20

July 30th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imeamuru shule moja ya mmiliki binafsi ipunguze karo ya shule kwa asilimia 20.

Jaji James Makau ameiamuru shule ya SABIS ® International School – Runda ipokee asilimia 80 ya karo hadi pale Wizara ya Elimu itakapoamuru shule zifunguliwe tena.

Wazazi waliishtaki shule hiyo wakisema imeendelea kudai karo asilimia mia moja ilhali shule zilifungwa Machi 2020 kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19.

Wazazi hao walisema licha ya shule hiyo kuendelea kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao, bado kuna huduma kama vile mabweni ambayo wanafunzi hawatumii na hata hawabebwi wakienda shule kwa mabasi ya shule ilhali wanaitishwa karo yote.

Wazazi hao walilamikia mahakama kwamba hawapati huduma zile waliafikiana na shule hiyo kuhusu watoto wao.

Waliiomba mahakama ipunguze karo hiyo kwa asili mia 50 lakini katika uamuzi wake Jaji Makau akapunguza karo kwa asilimia 20.

Pia jaji huyo amewaruhusu wazazi hao watumie herufi SPG kuwasilisha kesi hiyo ndipo wakinge wana wao dhidi ya kudhulumiwa.

Wazazi wote walitia sahini fomu ambayo iliyoonyesha huduma wanao watakuwa wakipata shuleni.

Ikipinga kesi hiyo shule hiyo ilisema mahakama haiwezi kuingilia masuala ya karo inayotozwa wanafunzi kwa “vile ni mkataba wa kibinafsi kati ya wazazi na shule.”

Mahakama ilisema ijapokuwa kuna mkataba wa kibinafsi, wazazi hawapati haki zao ipasavyo kwa vile wana wao hawaendi shule bali wanatumiwa masomo kwa mitandao na huduma wanazopata kwa walimu moja kwa moja hazipo.

Alisema kesi ya wazazi hao iko na mashiko kisheria na kusitisha agizo walipe karo yote.

Kesi itatengewa siku ya kusikizwa.