Shule ya Sheikh Khalifa kufanya hafla maalum ya kuomboleza kiongozi aliyeianzisha

Shule ya Sheikh Khalifa kufanya hafla maalum ya kuomboleza kiongozi aliyeianzisha

NA FARHIYA HUSSEIN

SHULE ya Upili na Ufundi ya Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan iliyo katika Kaunti ya Mombasa, imepanga kuandaa hafla maalumu ya maombolezi ya aliyekuwa Rais wa Milki za Kiarabu Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan.

Sheikh Khalifa ndiye mdhamini wa shule hiyo ambayo imekuwa ikipata matokeo bora katika Mitihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) kwa zaidi ya miongo miwili.

Naibu Mkuu wa Shule, Sheikh Rishard Rajab alisema wanahisi wamepoteza baba kufuatia kifo cha mfalme huyo.

“Tunajiona mayatima. Alikuwa sehemu ya maisha yetu kwa muda mrefu, hakika tumempoteza mlezi,” akasema.

Sheikh Rajab aliongeza kuwa siku ya utoaji zawadi kwa wanafunzi waliotia fora iliyokuwa ifanyike mwezi huu imeahirishwa kufuatia tangazo la UAE la kuomboleza kwa siku 40.

Rais Uhuru Kenyatta, alituma rambirambi zake kwa taifa la UAE na kumtaja marehemu kama kiongozi aliyekuwa na maono yaliyostawisha maendeleo Uarabuni kwa kiwango kikubwa.

Viongozi wa Mombasa wakiongozwa na Gavana Hassan Joho walimuomboleza marehemu kama kiongozi aliyejitolea kusaidia kuboresha masuala ya kijamii Mombasa.Bw Joho alimtaja marehemu kuwa kiongozi mwenye maono.

“Daima alikuwa na maslahi ya watu moyoni mwake. Atakumbukwa kwa ukarimu wake wa kupigiwa mfano kwa wahitaji na yatima duniani kote. Anaacha sifa ya kuigwa,” akasema Bw Joho.

Kwa upande wake mfanyabiashara na mwanasiasa Suleiman Shahbal alisema watu wa Mombasa walionufaika sana kupitia kwa udhamini wa marehemu Sheikh Khalifa.

Sheikh Khalifa alifariki Ijumaa, akiwa na umri wa miaka 73, kwa mujibu wa habari kutoka kwa Miliki ya UAE.

Alikuwa rais hadi kifo chake, lakini alionekana hadharani mara ya mwisho mwaka 2014 baada ya kuugua kiharusi.

Kaka yake, Mwanamfalme Mohammed Bin Zayed, aliingia mamlakani kama kaimu mtawala na alikuwa akiongoza maamuzi makubwa ya kigeni.

Sheikh Khalifa alikuwa Amiri wa Abu Dhabi, na kamanda mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu. Alikuwa mkuu wa wamajeshi kutoka mwaka wa 2004 hadi 2022.

Pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Petroli kutoka mwaka wa 1980.

UAE itaomboleza kwa siku 40 na bendera itapeperushwa nusu mlingoti. Kiongozi huyo alizikwa Ijumaa jioni.

  • Tags

You can share this post!

TALANTA YANGU: Matunda ya mfumo wa CBC

Kibai, Rono watwaa dhahabu Olimpiki ya Viziwi

T L