Lugha, Fasihi na Elimu

Shule yakabili ukeketaji ikipigana na mabadiliko ya tabianchi

May 18th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

MAMIA ya wasichana ambao wameokolewa kuepuka ukeketaji na ndoa za mapema wananufaika kwa kupata elimu katika Shule ya Wasichana ya St Elizabeth Morpus iliyoko Kaunti ya Pokot Magharibi huku wakipigana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti.

Shule hiyo mbali na kutoa elimu, hutumika kama kituo cha kuokoa wasichana wanaohangaishwa na minyororo ya mila zilizopitwa na wakati.

Mashirika mbalimbali yanashirikiana na shule hiyo kuwapiga jeki wasichana hao kukata kiu ya elimu huku nao wakichangamkia program za upanzi wa miti.

St Elizabeth Morpus ilianza mwaka wa 2008 na wakati huo ilikuwa na miti michache mno lakini sasa inajivunia maelfu ya miti ambayo imepandwa.

Mafanikio haya yamewezeshwa na mpango wa ufadhili kutoka kwa mashirika ya International Tree Foundation (ITF), Perur Rays of Hope na Lab Women.

Chini ya mpango huo, mashirika hayo yaalenga kupanda miche ya miti 100,000.

Mpango huo unahusisha upanzi wa miti kwenye nasari ambapo miche na pia miti inayokomaa huuzwa kwa mpangilio na kuleta mapato ambayo hupiga jeki ulipaji wa karo.

Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya St Elizabeth Morpus, Bi Caroline Menach, ambaye amekuwa akiendeleza elimu ya watoto wasichana ambao wazazi wao hushindwa kuwalipia karo, anasema wasichana hao wanalea miche ya miti hadi iwe miti mikubwa.

“Leo tumepanda miche ya miti 3,000,” alisema Bi Menach wakati Taifa Leo ilitembelea sehemu ya ardhi inayotumika kwa shughuli hiyo ya upanzi wa miti.

Alisema kuwa kufikia sasa shule hiyo ina wasichana 70 ambao wanalipiwa karo kutokana na mpango huo.

Alisema kupitia mpango huo, shule nyingine jirani kwenye kaunti hiyo zimenufaika na miche ya miti zaidi ya 50,000.

Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya St Elizabeth Morpus wakipanda miche ya miti. PICHA | OSCAR KAKAI

Pia wamepiga jeki upanzi wa miti kwenye msitu wa Kapkanyar na mingine kwa maboma ya wanajamii.

“Tumeona mabadiliko kwenye shule yetu. Wanafunzi na walimu wanahakikisha kuwa kuna mazingira mazuri,” akasema.

Alisema kuwa wanataka kuchangia kwa mpango wa serikali wa kupanda miti 15 bilioni kufikia mwaka wa 2032.

“Hatua yangu ya kuhusisha wasichana wadogo kwenye upanzi wa miti imechochewa na agizo wa Rais,” alisema.

Mwalimu huyo mkuu alisema kuwa kuna hitaji kubwa la miti ya kiasili.

“Miti ya kiasili inahitaji maji kidogo na inavutia ndege na kuongeza rotuba kwenye mashamba,” alieleza.

Alisema kuwa kutokana na eneo hilo kuwa kame, wao hutoa udongo kutoka kwa msitu wa Kamatira.

“Tunahakikisha kuwa tuna udongo safi wa kupanda miche ya miti,” alisema.

Naibu Kamishina katika Kaunti ndogo ya Kipkomo Bi Shilla Imbanga Kipkomo aliwataka wanafunzi kupanda na kulea miti hata nyumbani kwao na pia kwao watakapokuwa watu wazima na kazi zao.

“Mabadiliko ya tabianchi yameharibu mambo mengi,” alisema Bi Imbanga.

Alisema kuwa wanaunga mkono juhudi za serikali za kulenga kuwa na asilimia 10 ya miti nchini.

“Huu ni mpango maalumu wa kuhakikisha kuwa tunazuia maporomoko ya tope na ardhi, lakini pia mmomonyoko wa udongo,” alisema.

Aliwataka wakazi kushiriki kwenye shughuli za upanzi wa miti katika maeneo ya mashinani na mijini kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha maporomoko ya tope na mafuriko.

“Miti husaidia kulinda maeneo ya milima yasiwe na maporomoko. Ukikata mti mmoja, panda miwili. Tunataka kila mwanafunzi apande miti. Watu waache kuchoma makaa,” alishauri.

Mkurugenzi wa elimu katika Kaunti ndogo ya Kipkomo Bw Evans Onyanja aliutaka umma kukumbaria upanzi wa miti ili kuzuia kuenea kwa jangwa.

Aliongeza kusema kuwa mpango huo utachochea wakazi kupanda miti mingi ili kuongeza kiwango cha miti katika eneo hilo.

Bw Robert Aleutum ambaye ni mkurugenzi wa tume ya kuajiri walimu (TSC) kwenye Kaunti ndogo ya Kipkomo alisema kuwa shule hiyo imekuwa kituo cha wasichana kutoka kwa familia maskini na zenye changamoto lakini sasa wanaendeleza upanzi wa miti wakikata kiu ya elimu.

[email protected]