Lugha, Fasihi na Elimu

Shule yalia matokeo licha ya kuwika Kilifi

January 10th, 2024 2 min read

NA MAUREEN ONGALA

SHULE ya upili ya wavulana ya Arabuko Forest iliyo Kaunti ya Kilifi, imetilia shaka matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023) licha ya kuibuka ya kwanza kaunti hiyo.

Mwalimu Mkuu, Bw Alawi Rashid, anadai kuwa matokeo ya mwaka huu hayatoi twasira kamili ya jinsi shule hiyo imekuwa ikifanya kila mwaka.

Bw Rashid alisema alama wastani ya B- ambayo shule hiyo ilipata ilikuwa ya chini mno ikilinganishwa na malengo yao katika mtihani wa kitaifa wa mwaka wa 2023.

“Kulingana na mtihani wa KCSE wa 2023, tunahisi kuwa kulikuwa na tatizo kubwa ambalo hatuwezi kujadili kwa undani kwa sababu tumeshtuka sana. Tulikuwa na matarajio makubwa lakini si alama ya B-. Tulitarajia watahiniwa wetu wafanye vizuri zaidi ikizingatiwa kuwa tulikuwa tumewatayarisha vilivyo mwaka 2023,” akasema Bw Rashid.

Katika miaka iliyopita, watahiniwa wa kwanza shuleni humo walikuwa wakijizoloea alama za A- lakini katika matokeo yaliyotangazwa Jumatatu, wanafunzi wanne walioongoza kwa alama ya B+.

Shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 97 na ilipata alama wastani ya 8.14 kinyume na matarijio yao ya 9.2

“Wanafunzi wetu bora walipata alama za chini ambazo hata wao wenyewe hawakutarajia. Kisha kuna wanafunzi ambao walikuwa hawafanyi vyema sana darasani ilhali walipata alama za juu. Hilo limetukanganya,” akasema.

Mwaka wa 2022 shule hiyo ilipata alama ya wastani ya 8.7 ambayo ni B.

Hata hivyo, alisema licha ya hayo wanajivunia kuwa wa kwanza Kaunti ya Kilifi na pia kuwa kati ya shule zilizoongoza kitaifa.

Mwaka huu wanafunzi 88 walipata alama za C+ na zaidi na hivyo kuwawezesha kujiunga na chuo kikuu.

Kwa upande mwingine Shule ya Upili ya Kitaifa ya Wasichana ya Bahari iliyo Kilifi ilikuwa na alama ya wastani ya 7.69 (B).

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bi Hamaro Sylvano, alisema kuwa walikuwa na watahiniwa 260 japo mmoja hakufanya mtihani kwani alikuwa mgonjwa. Kati ya hao, wanafunzi 192 watajiunga na chuo kikuu.

Shule ya Upili ya Kitaifa ya Wavulana ya Ribe ilipata alama ya wastani ya 6.9